VETA YAFADHILI WENYE ULEMAVU 195 KUJIFUNZA UFUNDI STADI


NA MWANDISHI WETU

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imefadhili jumla ya wenye mahitaji maalum (wenye ulemavu) 195 kujifunza mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vyake.

Ufadhili  huo umetangazwa, tarehe 23 Desemba 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, wakati akitoa taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi kwa ajili ya mwaka wa masomo unaoanza Januari 2026, katika ofisi za VETA Makao Makuu, jijini Dodoma.

CPA Kasore amesema VETA ina nia ya kuona watu wenye mahitaji maalum wakipata fursa nyingi za kujiunga na kujifunza ufundi stadi ili nao waweze kujikwamua kiuchumi na kushiriki kikamilifu shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Amesema VETA imeendelea kubuni na kutekeleza miradi ya mafunzo ya muda mfupi kwa kushirikiana na wadau ikilenga kundi hilo kunufaika na elimu na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na kutoa kipaumbele kwa makundi hayo wakati wa udahili kwenye mafunzo ya muda mrefu.

“VETA italipa ada za mafunzo kwa miaka yote ya mafunzo, kuanzia Ngazi ya kwanza hadi ya Pili kwa wanafunzi wote wenye mahitaji maalum watakaodahiliwa mwaka huu. Nia yetu ni kuhakikisha wenye mahitaji maalum wanaendelea kujiunga na vyuo vya ufundi stadi na kujifunza stadi mbalimbali bila kikwazo cha gharama za mafunzo, miundombinu na hata nyenzo za ujifunzaji,” amefafanua. 

Amesema VETA inaendelea na jitihada za kuboresha miundombinu ya mafunzo katika vyuo vyake, pamoja na kuwapa wakufunzi mafunzo maalum ya kuhudumia watu wenye mahitaji maalum (wenye ulemavu). 

Ametumia fursa hiyo kuwaomba pia wadau mbalimbali kuiunga mkono VETA, hasa katika kufadhili mafunzo kwa kundi hili katika nyakati mbalimbali, ikiwemo mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa miaka ijayo.

Post a Comment

0 Comments