NA MWANDISHI WETU, LONGIDO
Mkuu
wa Wilaya ya Longido, Mhe. Salum Kalli, amewaahidi wananchi wa Kata ya
Engarenaibor kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) litapeleka umeme katika
mradi wa maji uliopo Kijiji cha Mairowa, kwenye chanzo cha chemichemi ya
Engongu, ili kuwezesha uendeshaji wa mtambo wa kusukuma maji na kuhakikisha
huduma ya maji inapatikana wakati wote.
DC
Kalli alitoa ahadi hiyo leo Januari 20, 2026, alipokuwa akizungumza na wananchi
wa kata hiyo katika mwendelezo wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za
wananchi.
Wananchi
wa Engarenaibor walilalamikia tatizo la uhaba wa maji, wakibainisha kuwa chanzo
kikuu cha changamoto hiyo ni ukosefu wa nishati ya uhakika ya kuendesha mtambo
wa kusukuma maji.
Amesema
Meneja wa TANESCO Wilaya ya Longido tayari analifanyia kazi suala hilo na
amewahakikishia wananchi kuwa muda si mrefu umeme utafikishwa katika eneo la
mradi huo na kuanza kutoa huduma.
“Tunalenga
kuhakikisha maji yanapatikana wakati wote. Umeme utakapofikishwa kwenye chanzo
hiki, mtambo utaweza kufanya kazi muda wote na wananchi watapata huduma ya
uhakika ya maji safi na salama,” amesema DC Kalli.
Aidha,
amesema kuwa katika jitihada za Serikali kutatua changamoto ya maji katika Kata
ya Engarenaibor, Wakala wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini
(RUWASA) umepanga kutekeleza Mradi wa Maji wa Kareo katika mwaka wa fedha ujao,
ambao utahusisha ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 50,000.
Katika
hatua nyingine, DC Kalli amewahamasisha wananchi kujiunga na mpango wa Bima ya
Afya kwa Wote, akisema utawapunguzia gharama za matibabu na kuwawezesha kupata
huduma za afya kwa urahisi popote nchini.
Ikumbukwe
kuwa wakati wa kampeni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia
Suluhu Hassan, aliahidi kuwa ndani ya siku 100 za uongozi wake wa muhula wa
pili wa Awamu ya Sita, Serikali itahakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya
kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote.

0 Comments