NA MWANDISHI WETU, LONGIDO
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe. Salum Kalli,
amemuagiza Mkuu wa Idara ya Ardhi kufika mara moja katika Kata ya Engarenaibor
kushughulikia madai ya uvamizi wa eneo la Soko la Engarenaibor pamoja na
ugawaji holela wa viwanja kwa baadhi ya wananchi kwa matumizi binafsi, hali
inayotishia maslahi ya umma.
DC Kalli ametoa agizo hilo leo Januari 20, 2026, baada
ya kusikiliza kero za wananchi wa kata hiyo waliolalamikia vitendo vya baadhi
ya watu kuvamia eneo la soko, jambo linaloweza kusababisha wananchi kukosa eneo
la kufanyia biashara.
Akizungumza katika mkutano huo, DC Kalli alisema:
“Kaimu Mkurugenzi yuko hapa, nenda kamweleze Mkuu
wa Idara ya Ardhi aje mara moja. Wakae hapa watatue changamoto hii ya uvamizi
wa soko. Tunataka kuwa na soko la kisasa. Kama kuna mtu amevamia na kuweka
msingi ndani ya soko, uvunjwe.”
Ameeleza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha Kata ya
Engarenaibor inakuwa na soko la kisasa litakalowawezesha wananchi kufanya
biashara zao kila siku na kuwa soko la mfano kwa maeneo mengine.
Aidha, DC Kalli amesema kutokana na kukua kwa kasi kwa
Kata ya Engarenaibor pamoja na ongezeko la watu, kuna umuhimu wa kupanga
matumizi ya ardhi kwa kuzingatia mipango miji, ikiwemo kutenga maeneo ya mitaa,
barabara, soko, shule na huduma nyingine za jamii ili kuepusha ujenzi holela na
kuongeza mvuto wa kimwonekano wa kata hiyo.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya amesema
operesheni maalum itafanyika kwa lengo la kuwakamata wauzaji na watumiaji wa
dawa za kulevya, ikiwemo bangi na mirungi.
Kauli hiyo imetolewa kufuatia malalamiko ya wananchi
kuhusu baadhi ya vijana kujihusisha na matumizi ya bangi na mirungi hadharani,
hali inayosababisha mmomonyoko wa maadili na kujiingiza katika vitendo vya
kihalifu.
DC Kalli amesisitiza kuwa vitendo hivyo havikubaliki
na ametangaza marufuku ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya katika Wilaya
ya Longido.
.jpg)
.jpg)
.jpg)

.jpg)
0 Comments