Waziri wa Nishati wa Uganda kutembelea mradi Chongolean,Tanga
Na Mwandishi Wetu,
Dar es salaam
Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini kutoka nchini Uganda Dkt. Ruth Nankabirwa
yuko nchini kwa ziara rasmi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bomba la kusafirisha
mafura ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, ili kujionea
hatua zilizodfikiwa kwa upande wa utekelezaji nchini Tanzania sambamba na mwenyeji
wake Mhe. Deogratius Ndejembi.
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa Habari, Waziri wa Nishati Mhe.
Deogratius Ndejembi amesema, kupitia mradi wa EACOP utaleta manufaa makubwa
kwenye ajira, ambapo jumla ya ajira 12,000 zimetolewa kwa vijana na wananchi wa
Tanzania na Uganda wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Mhe. Ndejembi amesema mpaka sasa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la
Afrika Mashariki umefikia asilimia 79 na unatarajia kukamilika mwezi Julai mwaka 2026,
huku ukichochea ukuaji wa Uchumi na ongezeko la mapato kwa nchi za Tanzania na
Uganda, na kuongeza kuwa utakuwa na uwezo pia wa kusafirisha mapipa 246,000 kwa
siku pindi utakapokamilika.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini kutoka Uganda Dkt. Ruth
Nankabirwa, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa nia yake ya dhati kwenye utekelezaji wa mradi huu ambao
umekuwa na mafanikio makubwa na umeleta mapinduzi makubwa kwa nchi za Afrika
Mashariki.
Mhe. Dkt. Ruth amesema kuwa, kuna haja ya watu wote wanaotekeleza miradi ya
kimkakati kama hii wanaopatiwa ajira kuwa na utaratibu maalumu wa kuwatambua ili
inapokuja miradi mingine wawe wanapewa nafasi kulingana na uzoefu na uadilifu
walionao katika utendaji wa kazi huku akitolea mfano wa miradi ya gesi na umeme
inayotarajiwa kutekelezwa na nchi hizi mbili .
Mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani
Tanga una urefu wa kilomita 1,443 ambapo kilomita 296 ziko nchini Uganda, na kilomita
1,147 ziko nchini Tanzania ambapo kwa upande wa Tanzania kuna jumla ya vituo 4 vya
kusukuma mafuta na Uganda kuna vituo 2 na kufanya jumla ya vituo vya kusukuma
mafuta kuwa 6.
0 Comments