Na Magrethy Katengu, Dar es Salaam
Licha ya jitihada za Serikali katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na kufaulu mitihani yao, wadau mbalimbali wa elimu nao wameendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kutoa huduma ya masomo maalum kwa wanafunzi wanaohitaji kujiimarisha kwa muda mfupi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 11, 2026 jijini Dar es Salaam, Mbunge wa Kigoma Mjini, Baba Levo, amesema elimu haina mwisho, na kwamba kufeli siyo sababu ya kukata tamaa.
Baba Levo, ambaye ameanza rasmi masomo katika Kituo cha Brothers Academy, amesema alilazimika kuacha shule hapo awali kutokana na changamoto ya ada, lakini sasa ameamua kurejea masomoni ili kutimiza ndoto zake.
Ameeleza kuwa amevutiwa na kituo hicho baada ya kusikia sifa zake, akidai kuwa wanafunzi wengi wanaosoma hapo hufaulu vizuri katika mitihani ya Kidato cha Nne na cha Sita.
“Ndugu zangu, elimu haina mwisho. Kufeli siyo kuondoka, msikate tamaa. Brothers Academy hakuna kufeli; ukisoma kwa bidii ufaulu ni uhakika. Mimi kama Mbunge nimeshaanza kusoma na sijaona ugumu wowote,” amesisitiza Baba Levo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Brothers Academy, Robert Rwezaura, amesema taasisi hiyo ina vituo mbalimbali ikiwemo Banana Ukonga na Mbagala. Ameongeza kuwa fomu za kujiunga zinapatikana katika vituo vyote kuanzia leo.
Amehimiza wanafunzi waliomaliza mitihani au wanaotaka kusoma madarasa mawili kwa mwaka mmoja kujitokeza kwa wingi kujiunga na masomo hayo.


0 Comments