Na. Joyce Ndunguru, Kiteto.
Kila asubuhi, mwanadamu huamka na matumaini mapya, Wahenga walisema kupanga ni kuchagua, maneno hayo ya Wahenga yamejidhihirisha katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makame (Makame WMA) iliyopo Wilaya ya Kiteto, Mkoa wa Manyara.
Wananchi wa Makame WMA wamechagua njia ya kulinda rasilimali za wanyamapori na mazingira yake na kuzigeuza kuwa chanzo cha maendeleo yanayogusa jamii nzima. Katika, eneo hili uhifadhi si nadharia, ni wajibu, ni uchumi, ni maisha.
Makame WMA ni muunganiko wa vijiji vitano (5) vilivyoungana na kutenga maeneo yao kwa ajili ya shughuli za uhifadhi na utalii, vijiji hivyo ni Makame, Ndedo, Ngabolo, Katikati na Irkiushiobor. Vijiji hivi viliona umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali ya wanyamapori na misitu na kuamua kuzilinda na kuzisimamia rasilimali hizo. Hapa, wananchi wanasimamia na wananufaika moja kwa moja na mapato yatokanayo na shughuli za uhifadhi.
Akizungumza na mwandishi wetu, Februari 10, 2026, Mhe. Remidius Mwema, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto amesema shughuli za uhifadhi na utalii zinazofanyika Makame WMA zimegusa maisha ya wananchi wa Tarafa hiyo katika nyanja zote za maisha. Mhe. Mwema ameongeza kuwa wao kama Serikali wanajivunia sana uwepo wa WMA hiyo katika Wilaya yao.
“Jumuiya hii imekuwa na mafanikio makubwa na mchango wake kiuchumi na kijamii katika Wilaya ni mkubwa, Makame WMA imekuwa ya mfano na watu mbalimbali wanakuja kujifunza kuhusu uhifadhi na jamii hapa,” amesema Mhe. Mwema.
Kuhusu mafanikio ya Makame WMA katika nyanja ya elimu, Mhe. Mwema amesema Makame WMA imeweza kujenga miundombinu ya madarasa (24) katika Vijiji vya Ngabolo, Irkiushiobor na Katikati, ujenzi wa uzio katika shule ya Msingi Ndedo na ujenzi wa Mabweni katika Shule ya Sekondari Makame.
Pamoja na miundombinu hiyo, Makame WMA imeweza kuajiri walimu wa mkataba kwa kila Kijiji, kununua vitabu na kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa vijiji wanachama, amesema Mhe. Mwema.
Mhe. Mwema ameongeza kuwa huduma za afya imeendelea kuimarika kwa kuzingatia kuwa Makame WMA imeweza kujenga Majengo ya Mama na Mtoto katika Zahanati ya Makame, Jengo la maabara katika Zahanati ya Ndedo na Jengo la OPD katika Zahanati ya Ngabolo na Katikati, sambamba na kuajiri wahudumu wa Afya wa mkataba kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa vijiji wanachama.
Naye, Katibu wa Makame WMA, Bw. Supuk Olekao amesema shughuli kubwa za Jumuiya yao ni ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na misitu, uwindaji wa kitalii pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa vijiji wanachama. Sambamba na miradi ya maendeleo iliyotekelezwa, Jumuiya yao imeweza kutoa fedha kwa makundi maalumu kama wanawake na vijana kwa ajili ya kujiinua kiuchumi.
Akizungumzia kuhusu ushirikiano wa Makame WMA na Serikali, Bw. Olekao amesema Makame WMA imekua ikishirikiana kwa karibu na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika masuala mbalimbali yakiwemo masuala ya doria, ukusanyaji wa mapato pamoja na mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya uhifadhi na uendeshaji wa Jumuiya.
Kwa upande wake, Afisa Wanyamapori kutoka TAWA, Joseph Mnyari amesema TAWA inaendelea kutekeleza dhana ya ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi wa wanyamapori nchini kwa kuhamasisha wananchi kutenga maeneo na kuanzisha Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori.
Aidha, ameongeza kuwa uanzishwaji wa WMA unalenga kuwezesha jamii kunufaika na rasilimali ya wanyamapori kwa kuwezesha miradi mbalimbali ya maendeleo kutokana na mapato yatokanayo na shughuli za uhifadhi na utalii.
Makame WMA imeonyesha dhahiri kwamba nguvu ya uhifadhi iko mikononi mwa wananchi. Kupitia Jumuiya hii imejidhihirisha jinsi rasilimali za wanyamapori na mazingira zinavyoweza kunufaisha maisha ya kila mwananchi. Huu ni ushuhuda kuwa wananchi wakiutunza uhifadhi nao utawatunza na kubadilisha maisha yao.
0 Comments