NA MWANDISHI WETU
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani imetoa msaada katika kituo cha watoto wenye uhitaji cha New Faraja Orphanage kilichopo Mburahati na kufuturu pamoja na watoto hao katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi msaada huo kwa watoto hao, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa BRELA Prof. Neema Mori amesema kuwa, “Wazo la mwaka huu ni ‘toa ili upokee’ hivyo nasi leo hii tumeshiriki kwa kutoa vitu mbalimbali ambavyo ni mahitaji yao ya kimwili na ya shule ili waendelee kwenda kuyatumia nyumbani na shuleni wakiwa kama watoto wetu,” alisema Prof. Mori.
Aidha, Prof. Mori ameongeza kuwa, katika kusherekea Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu, BRELA imefanya kitu cha tofauti kwa kutoa muda kushiriki na wanawake wengine kusherekea, kupata elimu ya kukuza uchumi na kutenda matendo ya huruma ya kutoa kwa watoto wenye uhitaji.
Akirejea dira ya mwaka 2050, inayoanza rasmi kutekelezwa Julai mwaka huu, Prof. Mori alisema kuwa, BRELA imekuwa ikitembea na wazo la kuwa na ujumuishi katika kuwezesha kufikia ufanisi katika dira ya 2050, tunafahamu nguzo ya pili ya dira yetu inaangalia kujenga uwezo wa watanzania kwenye maeneo tofauti yakiwemo Ujasiriamali, Biashara, Vijana, Wanawake sambamba na kuwa na uwezo wa kuleta maendeleo katika jamii.
“BRELA tumejikita kutekeleza dira hiyo kwa kuchangia kwa sababu tunaamini kwamba BRELA ni kiungo muhimu katika kuchangia ukuzaji na ukuaji wa sekta binafsi nchini, hivyo tuko mstari wa mbele kuwezesha na kuhakikisha sekta binasi inakua kwa kuwawezesha wafanyabiashara sio tu kurasimisha biashara zao lakini pia kuhakikisha biashara zao zinakuwa bora zaidi.’’
Naye mlezi wa kituo hicho, Bw. Hamisi Suleiman, aliishukuru BRELA kwa msaada huo ambao umetolewa kwao na kusema kuwa ni kitu kikubwa ambao utawawezesha watoto hao kujikimu na kuziomba taasisi nyingine kuiga mfano huo.
“Tunaishukuru BRELA kutualika kama kituo, kufuturisha watoto yatima, hiki walichokifanya sio kidogo kwa mwenyezi Mungu na watarajie makubwa, tunawaasa taasisi nyingine kuiga mfano huu sio kwa mwezi huu tu bali hata siku nyingine kwa kuwaalika watoto hawa maeneo tofauti tofauti ili waweze kufurahi nao; leo tumefurahi sana,”alisema Suleiman.
Mahitaji yaliyotolewa ni pamoja na mafuta ya kupikia na kupaka, sabuni, sukari, unga wa sembe, mchele, maharage, madaftari, dawa ya mswaki.
Kituo hicho kinalea jumla ya watoto 120 ambapo wanaishi hapo kituoni wakiwemo wasichana 62 na wavulana 58 kati yao watoto 5 bado hawajaanza shule, wengine ni wanafunzi katika shule za msingi, sekondari na vyuo.
Siku ya wanawake duniani huadhimishwa kila mwaka duniani kote. Kauli mbiu ya mwaka huu ni Haki na usawa kwa Wanawake na Wasichana, Msingi jumuishi kufikia dira 2050 ambapo katika kuadhimisha siku hiyo, awali wanawake wa BRELA walijumuika na wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam katika sherehe za Mkoa na baadae walipata elimu ya fedha na uwekezaji.
0 Comments