Na Mwandishi wetu, GEITA
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka wananchi waliopo katika Halmashauri 40 zilizopo katika Mikoa 10 ya Arusha, Mwanza, Kagera, Mara, Singida, Shinyanga, Geita, Rukwa,Tabora na Simiyu waupokee na kuulinda Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania (PAMOJA) ili kuwanufaisha wanawake kiuchumi pamoja na kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia (GBV).
Dkt. Gwajima ametoa wito huo Machi 08, 2026 Mkoani Geita kwa wananchi wa mikoa hiyo 10 na Halmashauri zake 40 ambazo zinatekeleza mradi huo wa PAMOJA, mara baada ya kuuzindua rasmi mradi wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
“Mradi huu wa PAMOJA wa miaka mitano (5), wananchi na waratibu mkiupokea, kuutekeleza na kuulinda ipasavyo, utakuwa ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini,” amesisitiza Dkt. Gwajima.
Aidha, Waziri Gwajima amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu, kuhakikisha Sekretarieti ya Uratibu wa Mradi wa PAMOJA inaendelea kutimiza wajibu wake kwa weledi na ufanisi ili fursa za mradi ziwafikie na kuwanufaisha walengwa na kumtaka atoe taarifa za mradi kwa umma ili waujue kwani ni mradi uliowalenga wananchi.
Dkt. Gwajima amesema katika kuendeleza azma ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, Serikali ya Awamu ya Sita ikiongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inashirikiana na Mdau wa Maendeleo Benki ya Dunia ambayo imetoa mkopo wa Dola za Marekani Milioni 100 na Ruzuku ya Dola za Kimarekani Millioni nne (4) sawa na Shilingi Bilioni 262 ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huo nchini.
Mradi huo wa PAMOJA uliozinduliwa na Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima unatekelezwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto - Zanzibar ambapo utekelezaji wake ulianza rasmi 30 Aprili, 2025 na utafikia tamati Februari 28, 2029.
0 Comments