KIRUSWA AINGILIA MGOGORO MGODI WA AMAZONITE KARATU, ASISITIZA UZINGATIAJI SHERIA



Aelekeza utaratibu wa ulipaji deni la Sh1.4 bilioni

Aipa Zhao Hao masharti ya kutimiza usalama wa mgodi ndani ya wiki mbili

Karatu, Arusha

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa, ameongoza juhudi za Serikali kutatua mgogoro wa Mgodi wa Madini ya Vito aina ya Amazonite uliopo Kitongoji cha Mandagawa, Kijiji cha Quandeng, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, kati ya Kampuni ya Paradiso Minerals Limited na mwekezaji wa msaada wa kiufundi, Zhao Hao.

Akifungua kikao cha majadiliano, Dkt. Kiruswa amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha haki za pande zote mbili zinalindwa kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan Sheria ya Madini Sura ya 123 na Kanuni za Msaada wa Kiufundi za mwaka 2025.

Ili kutatua mgogoro huo, Dkt. Kiruswa ameelekeza kuwa Kampuni ya Paradiso Minerals Limited imruhusu mbia wake kuzalisha madini mpaka yatakapofikia kiasi cha makontena 70 ambayo ni sawa na kiasi cha shilingi bilioni 1.4 ambazo tayari kampuni ya Paradiso imeshalipwa na baada ya hapo, mkataba uliopo utasitishwa ili kuruhusu kuandaliwa kwa mkataba mpya utakaozingatia  matakwa kwa usahihi ya Kanuni za madini za Usaidizi wa Ufundi (TSA) za mwaka 2025.

Aidha, Serikali imeipa kampuni ya Paradiso muda wa wiki mbili kurekebisha mapungufu ya kiusalama mgodini, ikiwemo masuala ya usimamizi wa mazingira, usalama wa wafanyakazi, uwepo wa mpango rasmi wa uchimbaji, mpango wa kufunga mgodi pamoja na mkakati wa kuhamisha ujuzi kwa wazawa.

Dkt. Kiruswa amesisitiza kuwa msaada wa kiufundi una nafasi muhimu katika kukuza wachimbaji wadogo kwa kuleta teknolojia na utaalamu wa kisasa, lakini akaonya kuwa lazima utekelezwe kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Kwa upande wa Kampuni ya Paradiso Minerals Limited, wakili wake Sabato Ngogo amesema makubaliano ya awali yalitaka madini yote yanayozalishwa kuuzwa kwa bei ya shilingi 800 kwa kilo, na kwamba tayari kampuni imepokea shilingi bilioni 1.4 kama malipo ya awali.

Hata hivyo, Ngogo ameeleza kuwepo kwa changamoto baada ya Zhao Hao kuonesha nia ya kununua mawe makubwa yenye ubora pekee, huku mawe madogo yakikosa soko, hali inayohitaji mapitio ya bei ili kuendana na hali halisi ya soko.

Kwa upande wake, Wakili wa Zhao Hao, Wallace Mfuko, amesema malipo ya bilioni 1.4 yalikuwa yakifanyika kwa mfumo wa malipo ya kila mwezi ya shilingi milioni 100 bila kuzingatia uzalishaji halisi. Ameongeza kuwa mwekezaji wake anapendelea mawe makubwa kutokana na mahitaji ya soko, huku akipendekeza kuruhusiwa kwa uzalishaji wa miezi mitatu ili kufikia thamani ya fedha iliyolipwa kabla ya kufanya majadiliano mapya ya bei.

Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa Machi 17, 2026, Kampuni ya Paradiso Minerals Limited iliwasilisha maombi ya dharura katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuzuia usafirishaji wa madini yaliyo kwenye mgogoro. Mahakama ilitoa amri ya muda inayomzuia Zhao Hao kusafirisha madini hayo hadi shauri la msingi litakapotolewa uamuzi.

Awali, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Godson Kamyanda, alisema ukaguzi uliofanywa mgodini ulibaini uwepo wa hatari kubwa kwa mazingira, usalama wa wafanyakazi na mali. Kufuatia hali hiyo, ofisi yake ilisimamisha shughuli za uzalishaji Januari 19, 2026 hadi marekebisho yatakapofanyika.

Serikali imetoa wito kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini kuhakikisha wanazingatia matakwa ya Sheria wanapoingia Mikakati ya Usaidizi wa Kiunfundi na wawekezaji.

Post a Comment

0 Comments