Halmashauri ya Wilaya ya Longido imegawa hati 54 za kimila za
umiliki wa ardhi kwa wanawake na kutoa elimu ya ujasiriamali, uwekezaji na
usawa wa kijinsia ikiwa ni maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Duniani yanayoadhimishwa kila Machi 8.
Akizungumza Machi 2, 2026 wilayani humo, Mkuu wa Idara ya
Maendeleo ya Jamii, Bi. Grace Mghase, alisema kaulimbiu ya mwaka huu isemayo, “Haki
na usawa kwa wanawake na wasichana ni msingi jumuishi kufikia Dira ya 2050,”
imekuwa mwongozo wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazolenga kumwezesha
mwanamke kiuchumi na kijamii.
Alisema hati hizo ziligawiwa katika vijiji vya Orbomba na
Karao, hatua inayolenga kuwawezesha wanawake kumiliki rasilimali ardhi na
kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Mbali na hilo, alibainisha
kuwa wametoa elimu ya ujasiriamali na uwekezaji kwa wanawake, ikiwemo mafunzo
ya kuweka akiba na kujiunga na vikundi vya VICOBA ili kupata mitaji na
kukopeshana.
“Kama tunavyofahamu, wanawake ni nguzo muhimu katika jamii na
familia. Hivyo, tunapomwezesha mwanamke tunaamini kuwa tumeliwezesha Taifa kwa
ujumla. Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, tumekuwa tukitekeleza
shughuli mbalimbali za kutoa elimu kwa wanawake. Tumetoa elimu ya ujasiriamali
sambamba na utoaji wa hati za kimila za umiliki wa ardhi katika vijiji vya
Karao na Orbomba, ambapo jumla ya hati 54 ziligawiwa kwa wanawake,” alisema Bi.
Mghase.
Katika kukabiliana na changamoto za kijamii, Bi. Mghase
alisema elimu ya usawa wa kijinsia imetolewa kwa viongozi wa kimila wa jamii ya
Kimasai, kwa kuwa wana nafasi muhimu katika kupunguza vitendo vya ukatili dhidi
ya wanawake na watoto.
Aidha, elimu kuhusu madhara ya ukeketaji na athari zake kwa
elimu ya mtoto wa kike imetolewa katika vijiji vya Orbomba na Kimokouwa.
Sambamba na hayo, Bi. Mghase alisema waliandaa bonanza la
michezo lililowakutanisha wanawake watumishi, wanafunzi wa Chuo cha VETA na
Longido Sekondari. Bonanza hilo lilihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa
pete, mpira wa miguu na mashindano ya kutembea na magunia, ambapo washindi
walipatiwa zawadi. Lengo lilikuwa kuimarisha afya na kuhamasisha utamaduni wa
michezo miongoni mwa wanawake.
Kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia la Polisi, alisema wametoa
misaada kwa wanawake wanaoishi katika mazingira magumu katika Kijiji cha
Tingatinga. Vilevile, wanaendelea kutoa elimu ya msaada wa kisheria kwa makundi
mbalimbali ya jamii.
Katika mwendelezo wa maadhimisho hayo, Bi. Mghase alieleza
kuwa leo Machi 3, 2026 kutafanyika kongamano la wanawake wilayani humo
litakalowakutanisha wanawake wa kada mbalimbali kujadili changamoto na
mafanikio yao. Aidha, Machi 5, 2026 alisema watashiriki maadhimisho ya kimkoa
yatakayofanyika katika Uwanja wa Ngarenaro, mkoani Arusha, kwa kupeleka vikundi
vya wajasiriamali kuonesha bidhaa zao, kubadilishana mawazo na kutafuta masoko.
Aliongeza kuwa utoaji wa elimu utaendelea kwa wanafunzi wa
kike katika shule za sekondari za Kamwanga na Lekule ili kuwajengea uwezo wa
kujitambua, kujiamini na kufikia malengo yao.









0 Comments