Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MAWAZIRI wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), wametakiwa kutoka na kuwaeleza wananchi tathmini ya kile kinachofanywa katika utekelezaji wa Ilani ya CCM na miradi mingine ya maendeleo kila robo mwaka ili wananchi wajue kile ambacho serikali inatekeleza.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Komredi Khamis Mbeto Khamis alisema wananchi wanayo haki ya kujua kinachofanywa na serikali yao hivyo kila wizara iwe na utaratibu huo.
Mbeto aliwapongeza mawaziri ambao wamejitokeza na kueleza utekelezaji wa siku 100 za Rais Dkt. Hussein Mwinyi lakini hiyo haitoshi wanapaswa kuwa na utaratibu wa mara kwa mara wa kutoka na kuwaeleza wananchi utekelezaji na uwajibikaji wa serikali kwa wananchi.
"Rais Dkt. Mwinyi mara baada ya kuwaapisha mawaziri 15 Novemba 2025, aliagiza kila wizara kuanzisha utaratibu wa tathmini ya utendaji kila robo mwaka ili kila mwananchi apate kuelewa kinachofanyika" alisema Mbeto.
Alibainisha kuwa Rais Dkt. Mwinyi ana mipango thabiti ya kuleta maendeleo, uwazi na uwajibikaji na kila waziri ni kigezo kinachofanikisha lengo hilo.
Mbeto alisema anayotekeleza Rais Dkt. Mwinyi yote yapo katika Ilani ya CCM na utekelezaji wake tunauona.
Alisema mpango wa mawaziri kuwaeleza wananchi tathmini ya
utekelezaji kupitia vyombo vya habari ni endelevu na sio kwa siku 100 pekee
toka iingie madarakani na CCM ambayo ndio inaisimamia serikali itawahoji
mawaziri kuhusu mpango huo, lengo likiwa wananchi kuelewa hatua zinazochukuliwa
kutatua changamoto zao.

0 Comments