MBETO: RAIS DK MAGUFULI AMEKUFA KIWILIWILI FIKRA ZAKE BADO ZINAISHI

Na Mwandishi  Wetu,Zanzibar 


Chama Cha Mapinduzi kimesema Marehemu Rais  John  Joseeph  Magufuli alikuwa  Kiongozi shujaa na Mzalendo  kwa Taifa lake wakati  wote wa maisha yake kabla na baada ya kuwa Rais. 

Pia kimesisitiza  juhudi na ushujaa wa kiongozi huyo, uliifanya Tanzania kuingia katika orodha ya nchi zenye Uchumi wa kati.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati  Maalum ya NEC  Zanzibar , Idara ya Itikadi , Uenezi na Mafunzo , Khamis  Mbeto Khamis alipozungumza na Kituo kimoja cha Habari Kisiwani unguja 

Mbeto  alisema katika uongozi wake kabla ya umauti  kumfikia, alimtaja Dk Magufuli  ndiye aliyeanzisha Ujenzi wa Reli ya Mwendokasi, Bwawa la kufua Umeme wa Maji , Ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi ,utengenezaji wa Vivuko , Meli mpya  Ziwa Victoria na kuiptia  Mikataba ya Migodi  ya  Madini.

"Ujasiri wa Rais Magufuli utakumbukwa milele.  Kimekufa kiwiliwili chake ,fikra na maono yake vitabaki. Alibuni mambo akayasimamia hadi yalipotoa matokeo  chanya. Alifanya   mengi akingozwa na  shime ya Uzalendo'  Alisema Mbeto .

Aidha Katibu huyo Mwenezi  alisema katika mambo ambayo Watanzania watayakumbuka , ni kiongozi huyo kufanya uamuzi  wa Serikali   yake kuhamishia Makao Makuu ya nchi kuwa Jijini Dodoma .

Alisema toka Awamu ya Kwanza uamuzi wa Serikali  ya Rais Mwalimu  Julisu Nyerere,  ulipitisha Azimio la  Makao Makuu kuhamishiwa Dodoma lakini kwa miaka yote azimio hilo halikuwezekana hadi  Awamu ya Tano chini ya Dk Magufuli .

Mbeto aliongeza kusema Dk Magufuli aliongozwa zaidi na Uzalendo ,uaminifu na Upendo kwa nchi yake ,   kwani alipiga vita  hadharani  uzembe ,ufisadi na ukwapuzi wa mali za Umma bila kumuonea yeyote  muhali.

"Utumishi wake wa muda mfupi  madarakani  umeacha alama na athari nyingi za kimaendeleo. Kiongozi huyo atakumbukwa kwa ujasiri wake wa kusimamia tunu za  Amani, Umoja na Mshikamano wa Taifa" Alisisisitiza

Pia Mbeto alisema muda wote katika uongozi wake alisimama kidete kuhakikisha rasilimali za Taifa zinainufaisha nchi kimaendeleo  huku akipiga vita maadui Ujinga ,Umasikini na Maradhi  kwa vitendo . 

"Hakumuonea aibu kiongozi  yeyote alipoonyesha kutosimamia vyema maslahi  ya Taifa. Alimtumbua yeyote bila woga na kuteuwa wengine  .Pia alihakikisha rasilimali na Vitega uchumi vya kisiasa  vinakinufaisha chama chake  "Alieleza  Mbeto 

Hata hivyo Katibu huyo Mwenezi  alisema Dk Magufuli akiwa madarakani  ndiye aliyefufua Shirika la  Ndege la ATCL kwa Serikali yake kununua Ndege mpya, Ujenzi  wa Daraja la Tanzanite, barabara  nyingi za lami na madaraja ya juu.

"Dk Magufuli  hakuendekeza  urafiki  au kujuana. Alihakisha katika  Serikali kunakuwepo nidhamu, uchapakazi na utumishi wenye maslahi  kwa Taifa. Aliitazama  nchi kwanza  kuliko kitu chochote " Alieleza Mbeto

Post a Comment

0 Comments