Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Kituo cha Uzalishaji wa Mbegu Bora za Miti na Vipando Morogoro, umepanda miche ya miti 1,005 katika vyuo vya ualimu Dakawa na Mhonda, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na jitihada za kulinda na kuhifadhi mazingira.

Akizungumza baada ya zoezi hilo, Mkuu wa Kituo hicho, Mhifadhi Mkuu *Mohammed Msalu*, alisema TFS inaendelea na juhudi za kupanda miti kila mwaka ili kurejesha uoto wa asili unaoharibika kutokana na shughuli za kibinadamu.

Alisema kwa mwaka, takribani hekta 23,400 hupandwa miti nchini, huku takwimu zikionyesha zaidi ya hekta 405,000 za misitu hupotea kila mwaka kutokana na shughuli kama kilimo, ufugaji, ujenzi wa makazi na uchomaji mkaa.

“Juhudi hizi haziwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa wadau wote. Tunahitaji taasisi za umma na binafsi pamoja na jamii kushiriki kikamilifu kudhibiti uharibifu wa misitu na kuongeza kasi ya upandaji miti,” alisema Msalu.

Kwa upande wake, mwanamuziki na Balozi wa Mazingira, *Seleman Msindi maarufu Afande Sele*, alisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa sheria na sera za mazingira ili kudhibiti vitendo vya uharibifu wa misitu.

Alisema siku hiyo ni muhimu kwa sababu inalenga kulinda uhai wa binadamu na mazingira, huku akitoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu katika upandaji na utunzaji wa miti ya asili.

“Tunapanda miti si kwa ajili ya leo tu, bali kwa ajili ya kesho. Ni wajibu wetu tuliorithishwa kuhakikisha tunalinda mazingira kwa vizazi vijavyo,” alisema.

Walimu wa vyuo vilivyohusika katika zoezi hilo walieleza kuwa wataendelea kuhamasisha wanafunzi kushiriki katika uhifadhi wa mazingira, wakitambua mchango wa miti katika kuboresha hali ya hewa na maisha ya jamii.

Zoezi hilo ni sehemu ya maadhimisho yanayoendelea kitaifa yenye lengo la kuongeza uelewa na ushiriki wa jamii katika kulinda rasilimali za misitu kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Post a Comment

0 Comments