Dodoma
Katika juhudi za kuimarisha utendaji kazi na ustawi wa watumishi, Wizara ya Madini imeendesha mafunzo maalum kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi, yakilenga kuwajengea uwezo katika masuala ya ulinzi wa taarifa binafsi pamoja na kuwahamasisha kuhusu fursa za uwekezaji kupitia UTT AMIS (Unit Trust of Tanzania – Asset Management and Investor Services).
Akizungumza leo Machi 23, 2025 wakati akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Festus Mbwilo amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wajumbe hao kama wawakilishi wa watumishi wenzao ili kuzingatia miongozo ya Serikali.
Akiwasilisha mada kuhusu taarifa binafsi, Afisa Tehama kutoka Wizara ya Madini Experansia Biseko amesisitiza umuhimu wa kulinda taarifa binafsi za watumishi na taasisi, akibainisha kuwa usimamizi sahihi wa taarifa ni nguzo muhimu katika kuimarisha uwajibikaji, uaminifu na ufanisi katika utumishi wa umma. Ameongeza kuwa, katika zama za teknolojia na mifumo ya kidijitali, ulinzi wa taarifa si chaguo bali ni wajibu wa kila mtumishi.
Kwa upande wa uwekezaji, Afisa Mwandamizi kutoka UTT AMIS Ahmed Salmin alipata nafasi ya kuwaelimisha washiriki hao kuhusu huduma na bidhaa zinazotolewa na UTT AMIS, ikiwemo mifuko ya uwekezaji inayowezesha watumishi kukuza kipato chao kwa njia salama na yenye tija. Ilielezwa kuwa uwekezaji ni nyenzo muhimu katika kujenga uhakika wa kifedha wa muda mfupi na mrefu.
Wajumbe wa Baraza hilo wameeleza kuridhishwa na mafunzo hayo, wakiahidi kuyatumia maarifa waliyopata katika kuboresha utendaji wao pamoja na kuwahamasisha watumishi wenzao kuhusu umuhimu wa kulinda taarifa binafsi na kuwekeza kwa ajili ya mustakabali bora.
Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada endelevu za Wizara ya Madini katika kuhakikisha watumishi wake wanakuwa na uelewa mpana wa masuala ya kiutawala, kiteknolojia na kiuchumi yanayochangia maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla.
UTT AMIS ni kampuni ya uwekezaji inayomilikiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Hazina. Kazi yake kuu ni kusimamia na kutoa fursa za uwekezaji kwa wananchi na taasisi kupitia mifuko maalum ya uwekezaji (unit trust funds).
0 Comments