Na Mwandishi Wetu,Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi kimesema kabla ya muda wa madaraka kikatiba kumalizika Mwaka 2030 ,Serikali ya Rais Dk Samia Suhuhu Hassan itawapatia Watanzania katiba mpya.
Aidha chama hicho kimesisitiza hata Tume zilizokusanya maoni ya Wananchi za kina Jaji Francis Nyalali ,Jaji Robert Kisanga na ile ya Jaji Joseph Warioba, haikuwa ajenda ya upinzani .
Ufafanuzi huo umetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi , Uenezi na Mafunzo ,Khamis Mbeto Khamis kufuatia madai ya Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu aliyesema Katiba mpya si agenda ya CCM.
Akijibu mapigo hayo, Mbeto alisema Rais wa Awamu ya Pili Hayati Ali Hassan Mwinyi alikuwa Mwana CCM, Bunge la chama kimoja lilikuwa na Wabunge wa CCM pekee , lakini kwa kutojali maslahi ya Kisiasa , lilipitisha Sheria Namba 5 ya Vyama Vingi Mwaka 1992.
Alisema hoja ya Katibu Mkuu huyo wa ACT ambaye pia ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini wakati akiwa Bungeni, haikuzingatia ukweli wa historia wala nia njema ya Serikali za CCM na Wakuu wa Nchi.
"Ado ajenge hoja akiwa na rejea ya ushahidi kamilifu . Kudai kuwa hoja ya Katiba mpya si ya CCM huo ni uzushi na upotoshajia .Huenda wakati Sheria Namba 5 ya Mwaka 1992 ikipitishwa alikuwa anasoma shule ya Msingi " Alisema Mbeto .
Rais Dk Samia mwaka jana wakati akizindua kampeni za CCM kwenye Viwanja vya Tanganyika Peckers jimbo la Kawe Jijini Dar Es ,aliwaahidi Watanzania kabla ya kuondoka kwake madarakani kikatiba, Serikali yake itawapatia Watanzania Katiba Mpya.
Pia Mbeto alieleza inawezekana Ado hajawahi kuziona wala kuzisoma Ripoti za Tume ya Jaji Nyalali na Jaji Robert Kisanga ili kushuhudia uamuzi makini uliochukuliwa na Serilali ya CCM kuhusu Vyama vingi .
"Wananchi Asilimia 80 walipendekeza Mfumo wa chama kimoja uendelee.Asilimia 20 ndio iliotaka Vyama vingi.Kudai ajenda ya Katiba mpya si ajenda ya CCM ni kukosa kwake ufahamu " Alieleza
Mwenezi huyo alisema laiti serikali na chama cha CCM kingekuwa na ukiritimba kingelishikilia kuendelea na mfumo wa demokrasia ya chama kimoja kutokana na matakwa ya wengi.
Kadhalika Mbeto alisema hata kuundwa kwa Tume ya kukusanya maoni ya Warioba , baadae kuundwa bunge maalum la katiba, iliofanya kazi hiyo ni serikali ya Rais Jakaya Kikwete hadi ikaandikwa katiba pendekezwa.
"Mara kadhaa Rais Dk Samia amewahi kusema kwanza anataka kujenga nchi .Hoja ya katiba mpya haifutiki wala kuchakaa. Katiba mpya bila shibe , maendeleo na uchumi imara haitabadili maisha yao" Alisisistiza Mwenezi huyo.

0 Comments