PBPA YATUMIA MFUMO WA SCADA KUDHIBITI UPOTEVU WA MAFUTA




Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya mafuta, umeanzisha mfumo wa kisasa wa Supervisory Control and Data Acquisition (SCADA) unaolenga kudhibiti upotevu wa mafuta kutoka melini hadi kwenye maghala ya kuhifadhi.

Haya yameelezwa na Mkaguzi wa Mafuta wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Issa Khamis Mwitazy wakati wa maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo Aprili 21, 2026

Alisema Mfumo huo unasoma na kufuatilia kwa wakati halisi kiasi cha mafuta kinachopita kwenye mita za Serikali zilizopo katika bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, na kulinganisha na kile kinachopita kwenye mita zilizopo kwenye maghala ya wateja kwa wakati mmoja.

“Endapo kutakuwa na tofauti ya kiasi cha mafuta kati ya mita za Serikali zilizopo bandarini na yale yaliyopita kwenye mita zilizopo kwenye maghala ya wateja, mfumo unatoa taarifa mara moja na hivyo kurahisisha kuchukua hatua stahiki.”

Aidha, Mwitazy alisema mfumo huo pia umeongeza uwazi na udhibiti katika sekta ya mafuta kwa kusaidia kuzuia uchepushaji wa mafuta kutoka ghala moja kwenda jingine kinyume na utaratibu uliopangwa.

“Kutokana na ufanisi wa mfumo wa SCADA na utaratibu wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja umeanza kuvutia wadau wa kimataifa, ambapo nchi jirani zikiwemo Zambia na Malawi zimefika nchini kujifunza namna Tanzania inavyosimamia uagizaji wa mafuta kwa pamoja na kudhibiti upotevu wake.”

Naye Meneja wa Sheria wa PBPA, Lilian Rwegumbura alisema wametumia Wiki ya Nishati kutoa elimu kwa Wabunge kuhusu utaratibu wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja, unaohusisha kuagiza mafuta kwa mpango wa miezi miwili mbele hatua ambayo imesaidia nchi kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta.

“Mahitaji yanayoletwa mwezi wa nne ni kwa ajili ya mafuta ya mwezi wa sita, kwa utaratibu huo wa miezi miwili mbele umetufanya kuwa na uhakika wa uwepo wa mafuta kwa nyakati zote. Tukishapata mahitaji tunatangaza zabuni ambazo zinashindaniwa na wazabuni wa ndani na nje kwa gharama za usafirishaji. Zabuni zimekuwa zikishandaniwa kila mwezi katika mafuta ya petroli, dizeli, mafuta ya taa na ndege.

Post a Comment

0 Comments