NA VICTOR MASANGU,PWANI
Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zinatarajiwa kuwasili na kupokelewa April 18/2026 mwaka katika eneo la Mapinga Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani zikitokea katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, amesema kwamba maandalizi yote yamekamilika na kwamba mapokezi hayo yatafanyika katika Wilaya ya Bagamoyo, Kata ya Mapinga, katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtambani. Aidha, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki tukio hilo muhimu la kihistoria.
Aliongeza kuwa Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika halmashauri zote tisa za mkoa huo, ukiambatana na shughuli mbalimbali za maendeleo, zikiwemo uwekaji wa mawe ya msingi, ukaguzi na uzinduzi wa miradi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.” Kaulimbiu hiyo inahimiza ushirikiano, kudumisha amani na kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha maendeleo endelevu ya Taifa.
Aidha, amewakaribisha wananchi wote wa Mkoa wa Pwani na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli zote zitakazofanyika katika kipindi chote cha mbio za Mwenge mkoani humo.

0 Comments