SERIKALI YATANGAZA ELIMU YA MSINGI YA LAZIMA KUWA MIAKA 10



Dodoma — Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ametangaza kuanza kwa utekelezaji wa mfumo mpya wa elimu utakaofanya elimu ya msingi kuwa ya lazima kwa kipindi cha miaka kumi, akisema ni sehemu ya mageuzi makubwa yaliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akihitimisha hotuba yake ya bajeti bungeni, Dkt. Nchemba amesema mageuzi hayo ni ya kihistoria kwani mara ya mwisho mabadiliko makubwa ya mfumo wa elimu yalifanyika mwaka 1967, wakati elimu ya lazima ilipopanuliwa kutoka darasa la nne hadi la saba.

Amesema mabadiliko hayo hayaishii kuongeza muda wa masomo pekee, bali yanaambatana na maboresho ya kina yaliyokuwa yakihitajika kwa muda mrefu, ikiwemo kuboreshwa kwa mitaala na miundombinu ya elimu.

“Mheshimiwa Rais ameonyesha ujasiri mkubwa wa kufanya maamuzi haya bila kujali gharama ili kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu bora,” amesema Dkt. Nchemba.

Ameeleza kuwa maandalizi ya utekelezaji wa mpango huo yamefanyika kwa kiwango kikubwa, huku hatua zilizobaki zikiendelea kukamilishwa ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa wa mafanikio.

Katika kuimarisha elimu ya ufundi, amesema serikali imeongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya shule kutoka takribani tano zilizokuwepo awali hadi zaidi ya 300, zikiwemo shule za awali na za ufundi, ambapo nyingi zina mwelekeo wa masomo ya kihandisi.

Aidha, amesema ujenzi wa madarasa 79,000 umeondoa changamoto ya mfumo wa “second selection” uliokuwa ukiwanyima baadhi ya wanafunzi fursa ya kuendelea na masomo.

Amesisitiza kuwa upanuzi huo wa miundombinu utahakikisha kila mtoto anapata nafasi ya elimu na kuweka msingi wa kuzalisha wataalamu na viongozi wa baadaye.

“Mageuzi haya yataingia katika historia ya nchi yetu na yatakumbukwa kuwa yamefanyika chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema

Post a Comment

0 Comments