▪️Ataka watanzania waache tabia ya kujidogosha
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema katika kipindi kifupi cha uongozi wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameandika historia ambayo kwa namna yoyote haiwezi kufutika kutokana na magaeuzi makubwa aliyoyafanya.
Amesema historia hiyo inaandikwa kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa, uandishi wa dira mpya ya Taifa ya 2025, kubadilisha mfumo wa elimu, kujenga madarasa mengi na shule za elimu ya amali, kuanzisha Bima ya Afya kwa Wote, kupandisha bajeti ya kilimo na kuongeza upatikanaji wa huduma za umeme na maji kwa wananchi vijijini.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo jioni (Jumatano, Aprili 15, 2026) Bungeni jijini Dodoma, wakati akitoa hoja ya kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2026/2027.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameingia katika historia ya viongozi wachache wa Taifa letu waliopata heshima na bahati ya kuandika Dira ya Taifa 2050 pamoja na nyaraka nyingine muhimu za utekelezaji wa dira ikiwemo mpango wa maendeleao wa muda mrefu.”
Kwenye sekta ya elimu, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mageuzi makubwa ambayo hayajawahi kufanyika tangu mwaka 1967. “Tulikuwa na vyuo vya ufundi vitano tu kwa nchi na wote tulikuwa tunategemea vyuo hivyo tu. Lakini yeye amejenga shule za amali 103 ambazo 29 kati ya hizo ni za kihandisi tu. Amejenga madarsa na kuondo double sessions,” amesema.
Akielezea mafanikio kwenye sekta ya kilimo, Waziri Mkuu amesema: “Ili kuwezesha mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha kuongezeka kwa bajeti ya Wizara ya kilimo mara tano kutoka shilingi bilioni 270 mwaka 2020/2021 hadi shilingi trillioni 1.23 mwaka 2025/2026. Tumeshuhudia upatikanaji wa pembejeo za kilimo na ongezeko la matumizi ya mbolea.”
Amesema Mheshimiwa ametoa zaidi ya trilioni 1.2 za kujenga Mradi wa Gridi Imara ili kuondoa tatizo la kukatikatika kwa umeme katika maeneo mbalimbali nchini.


0 Comments