MBETO AMPASHA OMO UCHAGUZI MKUU ZBAR UMESHAFANYIKA

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Chama Cha Mapjnduzi kimemtaka Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masuoud Othman, kutowapotosha Wananchi kwa kudai kuna waliojipa Mamlaka   ilahali  kura zilizopigwa  ndizo zilizoiweka Serikali  madarakani .

 Kwa muktadha huo, CCM kimesikitishwa kumsikia kiongozi huyo akipotosha ukweli kuhusu   Uchaguzi Mkuu kama kwamba uchaguzi bado haujafanyika Zanzibar.

Kauli hiyo imetamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar,Idara ya Itikadi, Uenezi  na Mafunzo,  Khamis Mbeto Khamis,  aliyesema matamshi ya Mwenyekiti huyo   wa ACT Wazalendo yana    upungufu na  walakin.

Wakati akifungua kikao cha Kamati Kuu ya ACT Wazalendo Jijini Dar es Salaam, Othman alidai kuna waliojipa Madaraka huku wakishindwa kutenda haki na kutotimiza wajibu stahiki kwa Wananchi.

Akijibu madai hayo, Mbeto alisema hakuna Serikali Duniani inayojiweka Madarakani, bila kupata ridhaa na idhini ya Wananchi kupitia ushiriki wao katika demokrasia ya Uchaguzi.

Alisema jaribio la kutaka kuiaminisha jamii na dunia ya kwamba Serikali iliojiweka madarakani, hizo ni Ngenga, Varange na sarakasi za kisiasa, jeuri na ukaidi usio na maana wala mantiki.

"Tumeshiriki Uchaguzi Mkuu Dunia nzima ikitushuhudia. Wagombea Urais, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani wa Vyama vyote waliomba kura wakapigiwa .Chama kilichoshinda kilitangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar  hivyo ni makosa kudai kuna waliojiweka Madarakani"  Alisema Mbeto.

Aidha,Katibu Mwenezi  huyo alisema CCM imekiita  kitendo cha Othman kupita akidai mshindi amejiweka madarakani,  madai hayo  ni porojo na pambio zisizo na uzito wowote .

"Wenzetu kwa kutojua na kutaka kuendekeza malumbano majukwaani wamekuwa wakibeza maendeleo bila kushirikiana na serikali.  Wananchi wapo na wanashuhudia yaliofanyika. Kwa kubeza kwao wamejikuta wakidondoka kidemokrasia" Alifahamisha

Hata hivyo Mbeto alimtaka Othman akubali ukweli hakuwa na nguvu za kisiasa za kumshinda mgombea Urais waCCM, ambaye tayari ameleta maendeleo  yaliowaridhisha wananchi   miaka mitano iliopita .

"Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 umeshafanyika na matokeo yametangazwa. Kukaa na kudhani Uchaguzi Mkuu bado  haujafanyika  ni kujidanganya mwenyewe. Uchaguzi umekwisha, mshindi amepatikana na ameshaunda serikali  "Alisema katibu huyo Mwenezi.



Post a Comment

0 Comments