▪️*Asisitiza kuzingatiwa kwa sheria za Haki madini na Haki Ardhi

Na Mwandishi Wetu, Geita 

Serikali, kupitia Wizara ya Madini, imetoa maelekezo ya kusimamisha  shughuli za uchimbaji madini katika eneo la Kanyindo  lililopo Wilaya ya Chato  kwenye Leseni ya Kampuni ya Bagogogo ikiwa ni hatua ya kuhakikisha uzingatiaji wa  Sheria juu ya haki ardhi na haki madini.

Uamuzi  huo umetolewa leo Mei 3, 2026 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde mkoani Geita wakati akitatua mgogoro unaohusisha Kampuni ya Uchimbaji madini ya Bagogogo na wamiliki wa mashamba katika  Wilaya ya Chato Mkoani Geita.

Waziri  Mavunde, amesema kuwa kisheria haki ya ardhi na haki ya madini ni mambo mawili tofauti ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura 123 , mmiliki wa leseni haruhusiwi kuanza uchimbaji bila kufikia makubaliano na mmiliki wa ardhi na iwapo mmiliki wa haki ardhi atakapokataa kutoa ridhaa pasipo kuwa na sababu ya msingi,Sheria imempa mamlaka Waziri Wa Madini kutoa maamuzi juu ya suala hilo.

Waziri Mavunde ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu kwenye kusimamia  shuguli za uchimbaji madini  ili kupunguza migogoro hisiyo ya lazima katika Sekta ya Madini na kuongeza pia sheria haizungumzi kuhusu wamiliki wa mashamba kupewa hisa kwenye eneo la uchimbaji hisipokuwa makubaliano ya pande husika wenyewe kwa wenyewe.

Waziri Mavunde ameongeza kuwa kwa mujibu wa sheria ya ardhi imetafsiri kutohusisha madini na Nishati ya Petroli , hivyo madini yote yaliyopo chini ya ardhi   ni mali ya umma.

Waziri Mavunde amewataka wamiliki wa mashamba na wamiliki wa Kampuni ya Bagogogo na wachimbaji waendelee na utaratibu wa mazungumzo kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chato juu ya uendeshwaji wa zoezi la tathimini  ili pande zote zenye mgogoro kuwa na maelewano na kuendelea na taratibu za kisheria.

Kuhusu Kampuni ya Bagogogo , Waziri Mavunde ameitaka kusitisha shughuli za uchimbaji mpaka pale itakapo kamilisha taratibu za fidia kwa wahusika.

Mkutano huo wa kusuluhisha mgogoro  umeshirikisha watu mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa Geita, Mhe. Martine Shigela , Mkuu wa Wilaya ya Chato,Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Mbunge wa Jimbo la Chato Kusini , wataalam kutoka Wizara ya Ardhi , Wataalam wa Wizara ya Madini , Tume ya Madini pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa.