NA MWANDISHI WETU, LONGIDO
Serikali imetoa shilingi milioni 584,280,029 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Engikaret Wilaya ya Longido mkoani Arusha.
Hayo yameelezwa leo Mei 26, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe. Salum Kalli, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Engikaret wakati wa ziara ya kutembelea eneo la ujenzi wa shule hiyo katika Kijiji cha Engikaret.
Mhe. Kalli amempongeza Diwani wa Kata hiyo, Mhe. Mathayo Ndaiya Laizer pamoja na wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki usafi wa eneo la mradi huo ili kuruhusu ujenzi kuanza mara moja.
“Nikushukuru Mheshimiwa Diwani kwa kushirikiana na wananchi kufanya usafi katika eneo hili la ujenzi wa shule mpya ya sekondari. Fedha tayari zimeingia kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu. Nawashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi,” amesema Mhe. Kalli.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu Wilayani Longido kupitia ujenzi wa shule mpya za sekondari.
Amesema kabla ya kuingia madarakani, Wilaya ya Longido ilikuwa na shule za sekondari 11 pekee, lakini Serikali imefanikisha ujenzi wa shule tano ambazo ni Kamwanga, Mundarara, Kimokouwa, Noondoto na Sinya pamoja na Shule ya Wasichana ya Longido Samia.
“Kwasasa tuna kata 16 zenye shule za sekondari, na sasa Engikaret inakuwa kata ya 17 kupata shule ya sekondari baada ya fedha hizi kutolewa na kuingia rasmi kwa ajili ya ujenzi,” amesema Mhe. Kalli.
Pia ametoa rai kwa viongozi wa Serikali wa kata hiyo kwa kushirikiana na Diwani ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ubora na kwa wakati ili kuwa mfano kwa maeneo mengine.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Engikaret, Mhe. Mathayo Ndaiya Laizer, amesema wananchi wamepokea kwa furaha mradi huo kwani utasaidia watoto kupata huduma ya elimu karibu na makazi yao.
Amesema wananchi wako tayari kushirikiana kuhakikisha ujenzi wa shule hiyo unakamilika kwa haraka ili wanafunzi waanze masomo mwaka ujao.
Naye Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Mhandisi Philipo Paulo, amesema mradi huo utahusisha ujenzi wa jengo la utawala, madarasa nane, ofisi mbili, maktaba, jengo la TEHAMA, maabara za Kemia, Biolojia na Fizikia pamoja na vyoo vya wavulana na wasichana na tenki la maji la ardhini.
0 Comments