WAKILI MARATHON KUFANYIKA DODOMA OKTOBA 31







NA MWANDISHI WETU

Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kinatarajia kuwakutanisha mawakili, wanamichezo na wadau mbalimbali Oktoba 31, 2026 jijini Dodoma kupitia mbio maalum za Wakili Marathon, zitakazolenga kuchagiza utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi.

Akizungumza leo Mei 15, 2026 jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya marathon hiyo, Mwenyekiti wa TPBA, Bw. Addo Novemba, amesema kuwa tukio hilo linalenga kuhamasisha afya, michezo na mshikamano katika jamii.

Amesema viongozi na watu mbalimbali mashuhuri wanatarajiwa kushiriki katika marathon hiyo, akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, pamoja na mwanariadha nguli Alphonce Simbu.

Kwa mujibu wa waandaaji, gharama za ushiriki zitakuwa kati ya Shilingi 40,000 hadi 100,000 kulingana na aina ya ushiriki, huku watoto wakitengewa Fun Marathon maalum pamoja na vifaa vya kushiriki mbio hizo.

“Pamoja na kuwa wataalamu wa sheria na kutetea watu mahakamani, hata kwenye mbio pia tupo. Mimi binafsi nimejisajili kukimbia kilomita 21,” amesema Addo Novemba.

Kwa upande wake, mwanariadha mstaafu Juma Ikangaa, aliyemwakilisha Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania, amesema marathon hiyo itasaidia kuibua vipaji vya wanariadha mahiri nchini.

Aidha, amewahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo ili kuendeleza ushiriki wao katika michezo.

“Mchezo wa marathon ni mchezo mama, karibu kila mchezo unahusisha kukimbia kwa namna moja au nyingine,” amesema Ikangaa.

Post a Comment

0 Comments