Benki ya CRDB, Tawi la Namanga Wilayani Longido, Mkoani Arusha, leo Juni 22, 2026, imetoa elimu kuhusu huduma za mikopo kwa watumishi wa Ofisi za Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Longido.
Akitoa elimu hiyo katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, J.K. Nyerere, Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Namanga, Bi. Neema Laizer, amesema benki hiyo inatoa mikopo kwa watumishi wa Serikali kwa riba ya asilimia 16, huku muda wa marejesho ukiwa hadi miaka 12.
Bi. Laizer amewataka watumishi hao kukopa kwa malengo na kuhakikisha wanatumia mikopo hiyo kwa shughuli zenye tija na zinazoonekana, pamoja na kuzingatia uwezo wao wa kifedha kulingana na viwango vya mishahara yao.
“Wala msiogope, ukikopa mapema utaweza kuutumia mkopo wako vizuri na kuweza kuurejesha bila shida yoyote. Ushauri wangu ni kwamba unatakiwa kukopa ukiwa na malengo na kufanya kitu kinachoonekana,” amesema Bi. Laizer.
Aidha, amewasisitiza watumishi hao kuzingatia nidhamu ya matumizi ya fedha na kuepuka kukopa zaidi ya uwezo wao ili kuhakikisha mikopo hiyo inakuwa na manufaa katika maisha yao.
Mbali na mikopo kwa watumishi wa Serikali, Bi. Laizer amesema Benki ya CRDB pia inatoa mikopo kwa wafanyabiashara, ambapo miongoni mwa masharti ni mfanyabiashara kuwa na biashara halali pamoja na leseni ya biashara.
Ameongeza kuwa mfanyabiashara anayehitaji mkopo anatakiwa kuwa na mali isiyohamishika, akitoa mfano wa nyumba iliyokamilika kwa kiwango kisichopungua asilimia 80. Kwa mikopo hiyo, amesema riba ni asilimia 20 na muda wa marejesho ni kati ya mwaka mmoja hadi mitatu.
Vilevile, Bi. Laizer amesema benki hiyo inatoa mikopo wezeshi
kwa wanawake waliopo katika vikundi, ambapo mikopo hiyo hutolewa bila riba kwa
lengo la kuwawezesha kiuchumi.



0 Comments