Na OWM–TAMISEMI, Dodoma
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendesha mafunzo ya Muongozo wa Chakula na Ulaji kwa Maafisa Lishe kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara, yakilenga kuimarisha elimu ya lishe kwa wananchi ili kuboresha afya za jamii na kupunguza athari za lishe duni.
Mafunzo hayo yaliyofanyika leo Juni 25, hadi Juni 27, 2026 jijini Dodoma, yanalenga kuwajengea uwezo Maafisa Lishe wa Mikoa 26 ya Tanzania kuwa mabalozi wa elimu ya ulaji bora katika maeneo yao ya kazi, kwa kuwasaidia wananchi kuelewa makundi ya vyakula, upangaji sahihi wa milo na umuhimu wa lishe bora.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Bw. Luitfrid Nnally, amesema Maafisa Lishe wanapaswa kutumia taaluma na ujuzi wao kuwafikia wananchi kwa elimu sahihi itakayosaidia kukabiliana na utapiamlo na magonjwa sugu yasiyoambukiza yanayochangiwa na ulaji usiofaa.
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata lishe stahiki ili kujenga rasilimali watu yenye afya na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na ukuzaji wa uchumi.
"Maafisa Lishe wanapotoa elimu kwa wananchi wanapaswa kuhamasisha mabadiliko ya tabia za ulaji ili kuboresha afya, kuongeza ufanisi wa kazi na kupunguza magonjwa sugu yasiyoambukiza," amesema Bw. Nnally.
Kwa upande wake, Afisa Lishe na Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Bi. Maria Ngilisho, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Maafisa Lishe kusambaza elimu ya ulaji bora kupitia huduma za kijamii zinazotolewa katika halmashauri, vyombo vya habari na mifumo mingine ya utoaji huduma.
Amesisitiza kuwa elimu ya lishe inamhusu kila mwananchi, hivyo ni muhimu kuhakikisha ujumbe wa ulaji bora unawafikia wananchi wote ili kupunguza madhara yatokanayo na ulaji usiofaa.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza uelewa kuhusu Muongozo wa Chakula na Ulaji na kuimarisha juhudi za Serikali za kujenga jamii yenye afya bora, lishe imara na nguvu kazi yenye tija kwa maendeleo endelevu ya Taifa.




0 Comments