Na Mwandishi Wetu,Zanzibar
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, Mhe. Moh’d Ali Abdallah, ameushukuru uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa kufanya ziara katika Mkoa huo, akieleza kuwa hatua hiyo inafungua fursa mpya za ushirikiano wa kiuchumi kati ya pande hizo mbili.
Akizungumza na viongozi hao, Mhe. Abdallah alisema Mkoa wa Mjini Magharibi uko tayari kuimarisha mahusiano ya kibiashara na Mkoa wa Mbeya, hasa katika sekta ya mazao ya kilimo.
"Hii kwetu ni fursa ya kufanya biashara na Mkoa wa Mbeya. Kama mlivyopita katika masoko yetu mmeona viazi na mchele kutoka Mbeya. Karibuni muwekeze Zanzibar, tutawapa eneo maalumu na tutaandika wazi kuwa bidhaa hizo zinatoka Mbeya ili wanaohitaji mazao hayo wajue mahali pa kuyapata kwa bei ya jumla," alisema Mhe. Abdallah.
Aliongeza kuwa uwekezaji huo utasaidia kuongeza upatikanaji wa mazao kutoka Mbeya katika masoko ya Mjini Magharibi huku ukiwanufaisha wakulima na wafanyabiashara wa pande zote mbili kupitia masoko ya uhakika.
Ziara ya Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya inalenga kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala ya maendeleo pamoja na kutafuta fursa za ushirikiano wa kiuchumi na kijamii.

0 Comments