Na Victor Masangu, Pwani
Serikali mkoani Pwani imeipongeza Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani kwa kuweza kuwa na mipango madhubuti katika kuweka mazingira rafiki na mazuri ya ukusanyaji wa mapato ambayo yameweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuleta mabadiliko chanya katika kuwezesha utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Pili Mnyema wakati wa halfa ya kilele cha maadhimisho ya miaka 30 ya TRA ambapo katika ngazi ya Mkoa yalifanyika katika ukumbi wa shule ya uongozi Mwalimu Juliasi Nyerere Wilaya ya Kibaha na kuwakutanisha walipa kodi mbali mbali pamoja na wadau wa maendeleo, wananchi na viongozi wa viongozi wa dini.
Katika kilele cha maadhimisho hayo ambayo yalikuwa ya aina yake yalikwenda sambamba na kufuatilia matangazo yaliyokuwa yanarushwa moja kwa moja kufuatilia halfa ya utoaji wa tuzo za walipa kodi bora mbali mbali Tanzania ambazo zilikuwa zinatolewa na mgeni rasmi Rais Dkt. Samia Suluhu Hasssan Jijini Dar es Salaam.
Katibu Tawala huyo amesema kwamba TRA Mkoa wa Pwani wamekuwa mstari wa mbele katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ikiwa sambamba na kutoa elimu ya kutosha kwa wafanyabiashara mbali mbali ambayo yameweza kuwasaidia walipa kodi kuweza kufahamu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari hali amabyo imeweza kuleta tija zaidi ya kuongeza kazi ya ukusanyaji.
"Nawapongeza sana TRA Mkoa wa Pwani kwa kuweza kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake maana haikuwa safari nyepesi mmeweza kuvuka milima na mabonde kwa hali na mali kwa hiyo kwa upande wangu nawapongeza sana na mzidi kuendelea kukusanya mapato kwa ajili ya kuweza kuisaidia serikali kupata mapato yake kihalali ambayo yatakwenda katika kusaidia katika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo."amebainisha Katibu Tawala.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani Salim Makame amesema kwamba lengo lao kubwa ni kuzidi kuendelea kushirikiana bega kwa bega na walipa kodi wote na kuwawekea mazingira mazuri ambayo yataweza kuwasaidia katika kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
"Tumetimiza miaka 30 ya TRA tangu kuanzishwa kwake kwa hiyo kitu kikubwa sisi tutaendelea kushirikiana bega kwa bega na wadau pamoja na walipa kodi na kwamba kitu kikubwa zaidi tunaomba ushirikiano wenu ambao utaweza kutusaidia kwa upande wetu katika suala zima la ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo ya Taifa letu hasa katika kipindi hiki tunapoanza mwaka mpya wa fedha ,"amebainisha Makame.
Aidha Makame amempongeza kwa dhati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kupambana kwa hali na mali katika kuwahudumia wananchi wa Tanzania na kuahidi kuyatekeleza maelekezo na maagizo mbali mbali ambayo yametolewa na Rais na kwamba watayafanyia kazi ili kuwa na TRA iliyobora zaidi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani katika kuadhimisha kilele cha miaka 30 imeweza kufanya mambo mbali mbali ikiwemo kutoa msaada wa vifaa mbali mbali kwa wafanyabiashara, mama lishe, kutoa elimu ya mlipa kodi, pamoja na kukutana na wadau na walipa kodi ili kuweka mikakati ya pamoja ambayo itasaidia katika ukusanyaji wa kodi kwa hiari kwa maendeleo ya Taifa.
.jpeg)

0 Comments