Dar es Salaam. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) mwaka huu umebadili mfumo wake wa ushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kwa kuja na bidhaa na huduma mpya zinazolenga kuongeza thamani ya mazao ya misitu, kuhamasisha matumizi ya nishati safi pamoja na kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi.
Akizungumza Julai 1, 2026 katika banda la Wizara ya Maliasili na Utalii ndani ya viwanja vya Sabasaba, Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, DCC Emmanuel K. Wilfred, alisema taasisi hiyo imejipanga kuonesha sura tofauti mwaka huu kwa kuwasogezea wananchi bidhaa ambazo wengi hawajawahi kuzizoea katika maonesho hayo.
Alisema maonesho ya mwaka huu yanafanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Biashara ya Kimataifa, Fahari ya Tanzania”, huku TFS ikitumia fursa hiyo kuonesha mnyororo mpana wa thamani wa mazao ya misitu na nyuki.
“Mwaka huu tumekuja tofauti kabisa na miaka mingine kwa kuwaletea wananchi bidhaa ambazo hawajavizoea. Tumeleta bidhaa mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu na nyuki ambazo zitawapa wananchi uelewa na fursa mpya za kiuchumi,” alisema Wilfred.
Alisema miongoni mwa mambo mapya yaliyoletwa mwaka huu ni mbegu za miti migumu, tofauti na miaka iliyopita ambapo wananchi wengi walikuwa wamezoea kuona msisitizo ukiwekwa zaidi kwenye uzalishaji wa miti laini.
Kwa mujibu wa DCC Wilfred, hatua hiyo inalenga kubadili mtazamo wa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiamini kuwa miti migumu hupatikana tu katika misitu ya asili na maeneo ya pori.
Alisema sasa wananchi wanaweza kupanda miti hiyo katika maeneo yao, kuitunza na baadaye kuivuna kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa mbao, kwa kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali.
Mbali na bidhaa za misitu, DCC Wilfred alisema TFS pia imeleta bidhaa za asali zilizoongezwa thamani kwa lengo la kuboresha lishe na afya za watumiaji.
Alifafanua kuwa baadhi ya bidhaa hizo zinajumuisha asali zilizochanganywa na Royal Jelly, ambazo kitaalamu zimeonekana kuwa na virutubisho vinavyoweza kusaidia kuboresha afya.
Katika hatua nyingine, alisema taasisi hiyo pia inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi kupitia maonesho ya majiko ya kisasa yanayotumia kiwango kidogo cha umeme.
Alisema matumizi ya teknolojia hiyo yatasaidia kupunguza utegemezi wa mkaa na hivyo kupunguza shinikizo kwa rasilimali za misitu.
“Tunataka wananchi waone kuwa inawezekana kutumia nishati kidogo, kupata matokeo mazuri ya kupika na wakati huohuo kuchangia uhifadhi wa mazingira,” alisema.
Aidha, alisema katika banda hilo wananchi pia watapata fursa ya kujifunza kuhusu ufugaji nyuki kupitia shamba darasa lililoandaliwa pamoja na huduma mbalimbali zinazohusiana na sekta hiyo.
Aliwahimiza wananchi kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii ili kujionea bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na TFS pamoja na kupata elimu kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya misitu.


0 Comments