*Jinsi Bodi na Menejimenti ya TAWA wanavyojenga uwajibikaji unaozaa matokeo katika sekta ya uhifadhi.
Na Beatus Maganja
Kila tunapoona ofisi mpya zikijengwa, miundombinu ikiimarishwa au shughuli za uhifadhi zikizidi kuleta matokeo chanya, mara nyingi hupongeza kile tunachokiona kwa macho. Lakini je, mafanikio hayo yanatokana na bahati? Ukweli ni kwamba, miradi ya maendeleo haikamiliki kwa bahati, inahitaji viongozi wanaofuatilia, wanaokagua na kuhakikisha kila hatua ya utekelezaji inaleta thamani kwa rasilimali za umma.
Falsafa hiyo ndiyo ilijidhihirisha Juni 16, 2026, wakati Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mej. Jen. (Mst.) Hamis Semfuko, ilipofanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Mlele, mkoani Katavi. Ziara hiyo haikuwa ya kawaida, ilikuwa sehemu ya utamaduni wa uwajibikaji unaowafanya viongozi kuingia uwandani kujionea utekelezaji wa shughuli za uhifadhi na miradi ya maendeleo badala ya kutegemea taarifa za ofisini pekee.
Moja ya mambo yaliyojitokeza wazi ni umuhimu wa ushirikiano. Mazungumzo kati ya Bodi na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mlele yalionesha kuwa mafanikio ya uhifadhi yanategemea mshikamano kati ya TAWA, Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi. Huu ndio msingi unaowezesha rasilimali za wanyamapori kulindwa kwa ufanisi na manufaa yake kuwafikia Watanzania.
Katika ziara hiyo, Bodi ilitembelea Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Ipole (Ipole WMA) na kujionea namna ushirikiano kati ya TAWA, jamii na wadau wa uhifadhi kama ADAP na Panthera unavyoendelea kuimarisha uhifadhi huku ukichochea maendeleo ya wananchi. Huu ni mfano kwamba jamii zinaposhirikishwa kikamilifu, uhifadhi hugeuka kuwa chanzo cha maendeleo badala ya kuwa jukumu la taasisi pekee.
Vilevile, ukaguzi wa ujenzi wa Ofisi Jumuishi za Mapori ya Akiba ya Ugalla, Inyonga na Rukwa ulidhihirisha kuwa TAWA inawekeza katika miundombinu inayoongeza ufanisi wa watumishi wake. Ofisi bora si majengo ya kawaida bali ni nyenzo muhimu za kuimarisha uratibu, kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu na kuboresha usimamizi wa rasilimali za wanyamapori.
Sambamba na hilo, kikao cha Bodi na Maafisa pamoja na Askari wa Mapori ya Akiba kilibeba ujumbe mzito wa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma. Hii inaonyesha kuwa taasisi imara haijengwi kwa miundombinu pekee, bali pia kwa watumishi wenye weledi, nidhamu na moyo wa kuwahudumia wananchi.
Kwa mtazamo wa uchambuzi, ziara ya Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA katika Wilaya ya Mlele ilikuwa zaidi ya ratiba ya kiutawala. Ilikuwa ni uthibitisho kwamba uwajibikaji wa viongozi ndio unaohakikisha miradi inakamilika kwa ubora, ushirikiano unaimarika, watumishi wanapata mwelekeo sahihi na malengo ya uhifadhi yanaendelea kufikiwa.
Ama hakika maendeleo ya kweli hayawezi kutegemea fedha pekee. Yanahitaji viongozi wanaoingia uwandani, wanaofuatilia utekelezaji na wanaowajibika kwa kila hatua. Ndiyo maana tunaweza kusema kwa kujiamini kuwa miradi haikamiliki kwa bahati... inasimamiwa.



0 Comments