SERIKALI NA WAWEKEZAJI WATOA HUDUMA MIGODINI WAJADILI CHANGAMOTO NA MAFANIKIO KWENYE SEKTA YA MADINI





▪️Rais Samia apongezwa kwa mazingira rafiki ya uwekezaji

▪️ Wadau wapongeza hatua za serikali za kutatua changamoto

▪️Waziri Mavunde awataka Watanzania kuanza ujenzi wa viwanda vya bidhaa za migodini

▪️ Kampuni ya MANTRA yanuia
kuiweka Tanzania kwenye kumi bora ya wazalishaji wa Uranium Duniani

Dar es salaam

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya madini kupitia majukwaa ya majadiliano kwa lengo la kujenga sekta yenye ushindani, inayovutia uwekezaji na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Mhe. Mavunde ameyasema hayo katika kikao cha Mining Breakfast Briefing (MBB), kilichoandaliwa kwa ushirikiano wa Chemba ya Migodi Tanzania(TCM) na Wizara ya Madini, ambapo ametoa wito kwa wadau kuendelea kutumia majukwaa hayo kujadili fursa na changamoto zinazohusu sekta ya madini.

Amewashukuru viongozi na wanachama wa Chemba ya Migodi Tanzania kwa kuendelea kutoa nafasi ya Serikali na wadau kukutana na kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali ya sekta hiyo, huku akilipongeza Mantra Tanzania Limited kwa kudhamini kikao hicho.

Amesema ushiriki wa wadau katika majukwaa hayo unaonesha dhamira ya pamoja ya kujenga sekta ya madini yenye ushindani, inayovutia mitaji na teknolojia, pamoja na kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kikamilifu kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Serikali inathamini utaratibu huu wa kukutana na wadau wa sekta ya madini kupitia Mining Breakfast Briefing, kwa kuwa unatoa fursa ya kufanya mazungumzo yenye tija, kujenga uelewa wa pamoja, kupokea changamoto zinazojitokeza na kutafuta suluhisho kwa pamoja,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta hiyo katika kutatua changamoto zinazojitokeza na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuongeza uzalishaji, ajira, mapato ya Serikali na kutumia fursa hiyo kuwataka watoa huduma migodini kuchangamkia fursa ya ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za migodini.

“Ni vyema kuendelea kukutana mara kwa mara kupitia jukwaa hili muhimu, kwa sababu linatupa nafasi ya kusikilizana, kujadiliana na kutafuta suluhisho la changamoto zinazotukabili kwa pamoja,” amesema.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba, amewashukuru wadau wa sekta ya madini kwa kushiriki katika kikao hicho, akiwataka kuongeza ushirikiano na mshikamano katika kukuza sekta hiyo.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kutatua changamoto, kuchochea uwekezaji na kuhakikisha fursa zinazotokana na rasilimali za madini zinatumika kwa manufaa mapana ya Taifa.

Amesisitiza kuwa mawasiliano ya mara kwa mara kati ya Serikali na wadau yataendelea kuwa nyenzo muhimu katika kubaini changamoto mapema na kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chemba ya Migodi Tanzania, Mhandisi Philbert Rweyemamu, amemshukuru Waziri Mavunde kwa kuendelea kudumisha mahusiano mazuri na wadau wa sekta ya madini.

Amepongeza utaratibu wa Serikali kukutana mara kwa mara na wadau kupitia Mining Breakfast Briefing, akisema majukwaa hayo ni muhimu katika kujenga mawasiliano ya karibu, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto pamoja na fursa zilizopo katika sekta hiyo.

Amesema Chemba ya Migodi Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali chini ya uongozi imara wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan katika kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kuimarika, kuvutia uwekezaji na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

Akizungumzia maendeleo ya mradi wa Uranium, Meneja wa Uendelevu wa Mantra Tanzania Limited, Majani Wambura, amesema mradi huo umebaini uwepo wa hifadhi ya takribani tani 58,500 za Uranium, huku uzalishaji ukitarajiwa kufikia tani 3,000 kwa mwaka.

Amesema mradi huo unatarajiwa kutoa ajira kwa zaidi ya wafanyakazi 4,000 baada ya kuanza uzalishaji, hatua itakayochochea shughuli za kiuchumi na kuongeza fursa kwa Watanzania.

Kwa mujibu wa Wambura, mradi huo unatarajiwa kuanza uzalishaji mwaka 2029  na kuwa na maisha ya zaidi ya miaka 20, huku utafiti ukiendelea ili kubaini uwepo wa rasilimali zaidi katika maeneo yanayohusishwa na mradi huo ambapo hatua zote hizo zitaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa 10 wa Uraniaum Duniani.

Ameeleza kuwa Uranium ni rasilimali yenye matumizi mbalimbali, ikiwemo katika uzalishaji wa nishati ya umeme na sekta ya afya, hususan matumizi ya mionzi katika uchunguzi na matibabu.

Akifunga jukwaa hilo, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema Serikali na wadau wa sekta ya madini wanapaswa kuendelea kukutana mara kwa mara kupitia Mining Breakfast Briefing (MBB) ili kujadili na kutatua changamoto zinazojitokeza katika sekta hiyo.

Amesema mikutano ya mara kwa mara itasaidia kujenga mawasiliano na uelewa wa pamoja kati ya Serikali na wadau, kujadili changamoto na fursa zilizopo, pamoja na kuweka mazingira bora zaidi ya uwekezaji katika sekta ya madini.

Post a Comment

0 Comments