SERIKALI YAENDELEA KUKUZA MATUMIZI YA NISHATI JADIDIFU NCHINI


NA MWANDISHI WETU

Serikali imeendelea kuhimiza uendelezaji na matumizi ya nishati jadidifu kama sehemu ya mkakati wa kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika na endelevu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Akizungumza katika Kongamano la Siku ya Nishati (Energy Day) linaloendelea katika Ukumbi wa Mwandoro, Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere – Sabasaba, jijini Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Jadidifu, Mha. Imani Mruma, alisema nishati jadidifu ina mchango mkubwa katika kupanua upatikanaji wa nishati na kuharakisha maendeleo ya sekta hiyo.

Mha. Mruma alieleza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya vyanzo vya nishati jadidifu kupitia ubunifu, matumizi ya teknolojia na utekelezaji wa mikakati inayolenga kuongeza uwekezaji na upatikanaji wa nishati safi na endelevu.

Aliongeza kuwa juhudi hizo zinalenga kuhakikisha nishati jadidifu inachangia kikamilifu katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.



Post a Comment

0 Comments