Na Mwandishi Wetu, Arusha
SERIKALI imeeleza kuwa uhifadhi wa misitu umeendelea kuwa nguzo muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, huku ikisisitiza utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolinda bioanuai na kuimarisha ustahimilivu wa jamii zinazozunguka hifadhi za misitu.
Kauli hiyo ilitolewa Julai 9, 2026, katika Kituo cha Mikutano cha Ngorongoro Convention Centre mjini Arusha wakati wa Mkutano wa Tano wa Kamati ya Uendeshaji wa Mradi wa “Kuimarisha Ustahimilivu wa Bioanuai ya Misitu dhidi ya Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika Hifadhi za Mazingira Asilia Tanzania.”
Hotuba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii iliwakilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Bw. Daniel Charles Pancras, huku maelezo ya Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yakisomwa na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali TFS, Dkt. Zainabu Shaban Bungwa.
Akifungua mkutano huo, Serikali ilieleza kuwa Tanzania, yenye misitu inayokadiriwa kufunika takribani asilimia 55 ya eneo la nchi, ina wajibu wa kuhakikisha rasilimali hizo zinasimamiwa kwa uendelevu ili ziendelee kuwa kinga dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi na chanzo cha huduma muhimu za kiikolojia.
Aidha, Serikali iliipongeza TFS, UNDP na taasisi nyingine zinazotekeleza mradi huo kwa ushirikiano uliowezesha kufikiwa kwa mafanikio mbalimbali tangu mradi ulipoanza, huku ikitaka kasi ya utekelezaji iendelee ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Tunahitaji kuendelea kusimamia mradi huu kwa uwajibikaji, uwazi na uratibu mzuri. Utekelezaji kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa utaimarisha imani ya washirika wa maendeleo na kuhakikisha tunapata matokeo yanayotarajiwa,” ilieleza sehemu ya hotuba ya Katibu Mkuu.
Kwa upande wake, TFS ilieleza kuwa tangu mkutano uliopita uliofanyika Desemba 2025, shughuli nyingi zilizopangwa zimekamilishwa kwa mafanikio licha ya changamoto chache zilizojitokeza, zikishughulikiwa kwa ushirikiano wa wadau wote wa mradi.
Dkt. Bungwa alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya TFS, UNDP, Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI pamoja na taasisi nyingine zinazounda Kamati ya Uendeshaji wa Mradi.
Alisema mkutano huo unatoa fursa ya kupitia utekelezaji wa mpango kazi na taarifa ya fedha kwa kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu, kujadili changamoto zilizojitokeza na kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi katika hatua zinazofuata.
“TFS inaendelea kuwa na dhamira thabiti ya kutekeleza mradi huu kwa uwazi, ufanisi na kwa kuzingatia maelekezo ya Kamati ili kuhakikisha unaleta matokeo chanya kwa misitu, bioanuai na wananchi wanaonufaika na rasilimali hizi,” alisema.
Washiriki wa mkutano huo walijumuisha viongozi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, UNDP, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Wizara ya Fedha, wawakilishi wa Mikoa ya Arusha, Manyara, Lindi, Ruvuma na Pwani, pamoja na taasisi za uhifadhi zikiwemo TaFF, EAMCEF, TNC na MJUMITA.
Mradi huo unalenga kuongeza uwezo wa hifadhi za misitu ya mazingira asilia kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi bioanuai na kuimarisha ushiriki wa jamii katika usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu nchini.


0 Comments