NA MWANDISHI WETU
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Jumatano, Julai 1, 2026, amekagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, lililopo mjini Mugumu, mkoani Mara, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoani humo.
Akiwasilisha taarifa ya ujenzi huo, Msanifu Majengo wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Mara, Bw. Nicholas Jeje, alisema mradi huo unagharimu shilingi bilioni 4.5 zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alisema ujenzi ulianza Aprili 10, 2025 na unatarajiwa kukamilika Aprili 9, 2028, huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 42.
Alieleza kuwa jengo hilo litakuwa na ofisi 62, zikiwemo ofisi za Mkurugenzi wa Halmashauri na Mwenyekiti wa Halmashauri, pamoja na kumbi mbili za mikutano zenye uwezo wa kuchukua watu 50 na 110 mtawalia, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, alimkaribisha Waziri Mkuu mkoani humo na kusema ziara hiyo itamwezesha kutembelea wilaya zote sita, halmashauri zote tisa na majimbo yote 10 ya uchaguzi yaliyopo mkoani Mara, ambapo pamoja na mambo mengine atakagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.



0 Comments