Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imetenga sh.bilioni 22.06 katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kujenga vituo vinavyohamishika vya kusambaza gesi asilia iliyoshindiliwa (Mobile CNG Stations).
Lengo la kujenga vituo hivyo ni kuongeza upatikanaji wa gesi asilia katika mikoa iliyo mbali na miundombinu ya gesi hiyo.
Hayo yamesemwa na Mhandisi Gleam Ulungi katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Amesema usambazaji huo wa gesi asilia utafanyika kwa kutumia magari maalum ya kusafirisha gesi iliyoshindiliwa (CNG trucks) kutoka vituo mama vilivyopo Dar es Salaam na kuifikisha katika maeneo husika.
Amefafanua kuwa TPDC itasimika vituo vitano vya Mobile CNG, ambapo viwili vitajengwa mkoani Dar es Salaam, kimoja Morogoro na viwili Dodoma.
Aidha, amesema Serikali kupitia TPDC itaendelea kutafuta maeneo na kuanza kufanya tathmini ya athari kwa mazingira na jamii katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha kwa ajili ya ujenzi wa vituo viwili katika kila mkoa.




0 Comments