NA MWANDISHI WETU
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius J. Ndejembi, amepongeza kiwango kikubwa cha ushiriki wa Watanzania katika utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), akisema mradi huo umeendelea kuwa chachu ya ajira, uhamishaji wa ujuzi na ukuaji wa sekta binafsi nchini.
Akizungumza wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi huo katika Kituo cha Kupunguza Msukumo wa Mafuta cha Sindeni, wilayani Handeni mkoani Tanga, Waziri Ndejembi amesema ameridhishwa na namna Watanzania walivyoshirikishwa katika ngazi zote za utekelezaji wa mradi huo, kuanzia wahandisi hadi wafanyakazi wasio na ujuzi.
“Kilichoniridhisha zaidi katika mradi huu ni ushirikishwaji wa Watanzania katika kila hatua ya utekelezaji wake. Kuanzia wahandisi hadi wafanyakazi wasio na ujuzi ni Watanzania. Uzoefu na ujuzi wanaoupata utawajengea uwezo wa kushindana katika miradi mikubwa ya kimataifa,” amesema Waziri Ndejembi.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha utekelezaji wa mradi huo, jumla ya ajira 10,000 zimezalishwa, ambapo ajira 7,500 sawa na asilimia 75 zimetolewa kwa Watanzania. Amesema hatua hiyo imewajengea vijana uwezo wa kitaalamu na kuwapatia uzoefu utakaowawezesha kushiriki katika miradi mingine mikubwa ya kimkakati ndani na nje ya nchi.
Waziri Ndejembi amesema licha ya mradi huo kufikia hatua za mwisho za utekelezaji, fursa za ajira na maendeleo ya kitaalamu zitaendelea kuwepo wakati wa uendeshaji wa bomba hilo. Ameongeza kuwa Serikali inaendelea na maandalizi ya miradi mingine mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta yaliyosafishwa kutoka Tanga kwenda Uganda, ambalo lipo katika hatua za makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Uganda, pamoja na mpango wa kujenga bomba jipya la TAZAMA kwa ushirikiano na Serikali ya Zambia kutokana na bomba la sasa, lililojengwa mwaka 1968, kufikia mwisho wa maisha yake ya matumizi.
Aidha, Waziri Ndejembi amesema zaidi ya kampuni 200 za Kitanzania zimepatiwa kandarasi za ugavi wa bidhaa na huduma zenye thamani inayozidi Shilingi trilioni 1.325 kupitia mradi wa EACOP. Amesema hatua hiyo imeongeza ushiriki wa sekta binafsi ya ndani, imeimarisha uwezo wa kampuni za Kitanzania kushiriki katika miradi mikubwa na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.




0 Comments