BRELA YAKUMBUSHA KAMPUNI KUWASILISHA TAARIFA ZA MWAKA NA HESABU ZILIZOKAGULIWA

Dar es Salaam – 07 Agosti, 2026

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewakumbusha wamiliki, wakurugenzi na makatibu wa kampuni nchini kutekeleza wajibu wa kuwasilisha taarifa za mizania ya mwaka pamoja na hesabu za kampuni zilizokaguliwa kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa BRELA, uwasilishaji wa taarifa hizo (Annual Returns and Audited Annual Accounts) ni takwa la kisheria kwa kampuni zote binafsi na za umma, kwa mujibu wa Kifungu Na. 131 cha Sheria ya Makampuni, Sura ya 212 toleo la mwaka 2023.

BRELA imeeleza kuwa kampuni zinapaswa kuwasilisha taarifa hizo kwa Msajili wa Kampuni kila mwaka mara baada ya kufikia tarehe ya usajili wa kampuni (Anniversary of Incorporation) au tarehe nyingine yoyote iliyoidhinishwa na Msajili wa Kampuni.

Aidha, kampuni za kigeni (Foreign Companies) zinatakiwa kuwasilisha hesabu za mwaka pindi inapofika tarehe yao ya hesabu (Accounting Date) kama ilivyoainishwa kwenye taarifa za kampuni zilizowasilishwa BRELA.

Katika utekelezaji wa zoezi hilo, BRELA imeeleza kuwa uwasilishaji wa taarifa utafanyika kupitia mfumo ulioboreshwa wa BRELA Online System (BOS), ambapo mmiliki, mkurugenzi au katibu wa kampuni ataweza kuwasilisha taarifa hizo moja kwa moja kupitia mfumo huo.

Kwa watumiaji ambao bado wanatumia akaunti za mfumo wa awali wa ORS, wametakiwa kutumia barua pepe iliyotumika wakati wa usajili wa akaunti hiyo na kubonyeza sehemu ya “Forgot Password” ili kupata maelekezo ya kuwezesha kuingia kwenye mfumo wa BOS.

BRELA imeonya kuwa kampuni ambazo hazitakamilisha uwasilishaji wa taarifa hizo hazitaweza kufanya mabadiliko yoyote ya taarifa yanayowasilishwa kwa Msajili hadi pale zitakapokamilisha zoezi hilo.

Kwa maelezo zaidi au msaada wa mfumo, wananchi wametakiwa kuwasiliana na BRELA kupitia simu +255 (0) 22 2212800 au barua pepe support.bos@brela.go.tz.

Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, BRELA.

 


Post a Comment

0 Comments