NGORONGORO KIVUTIO CHA UTALII KILICHOTEMBELEWA ZAIDI MWAKA 2025.



NA MWANDISHI WETU

Eneo la hifadhi ya Ngorongoro limetajwa kuwa ndio kivutio namba moja kilichotembelewa zaidi na watalii kwa mwaka 2025 ambapo watalii 859,933 walitembelea hifadhi hiyo ambayo ni kivutio namba moja cha utalii barani afrika.

Kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyofanya  utafiti wa wageni wa kimataifa wakati wa kuondoka  mwaka 2025 (The 2025 International visitors Exit Survey report) inaOnyesha kuwa eneo la hifadhi ya Ngorongoro limetembelewa na asilimia 14.2 ya wageni waliowasili chini kwa mwaka huo na kuwa kinara katika maeneo yote ya utalii nchini.

Ongezeko la idadi ya wageni katika hifadhi ya Ngorongoro na maeneo mengine ya nchi inatokana na jitihada za serikali na wadau wa utalii kuendelea kuitangaza Tanzania katika majukwaa na maonesho ya kimataifa huku Ngorongoro ikiboresha huduma za wageni na kuimarisha miundombinu ya utalii kwenye vivutio vilivyopo ndani ya hifadhi ili kuongeza mtawanyiko wa wageni kwenye vivutio hivyo.

Eneo la hifadhi ya Ngorongoro lina vivutio mbalimbali ikiwemo kreta tatu za Ngorongoro, Olmot na Empakai, Vivutio vingine ni pamoja na mazalia ya nyumbu ndutu, mchanga unaohama, maporomoko ya maji endoro, mapango ya tembo, mlima Lolmalasin, jabali la nasera, msitu wa nyanda za juu kaskazini, makumbusho ya olduvai na nyayo za Laetoli zenye umri wa miaka milioni 3.6 iliyopita.

Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lililoanzishwa mwaka 1959 lenye ukubwa wa kilomita za mraba 8,292 lina hadhi tatu zinazotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), ambazo ni; Man and Biosphere Reserve (Hifadhi ya Binadamu na Baiolojia), Mixed World Heritage Site (Urithi wa dunia Mchanganyiko), Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark (Hifadhi ya Jiolojia ya Dunia), Aidha, mwaka 2023 na 2025, Hifadhi ya Ngorongoro ilichaguliwa na Mtandao wa World Travel Awards (WTA) kama Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika (Africa’s Leading Tourist Attraction).

Post a Comment

0 Comments