Na Mwandishi Wetu,Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi kimesema kinaridhishwa na juhudi mahususi zilizochukuliwa hatua kwa hatua , na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuelekea ,hatimaye kupata Muafaka, suluhu na Maridhhano ya Kitaifa .
CCM pia kimeutaja uamuzi wa Rais kuanza kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii, Wanataaluma, Viongozi wa Dini Wanasiasa, Uundaji wa Tume za Haki Jinai na Tume ya Uchunguzi ni hatua endelevu .
Hayo yamebainishwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi ,Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, aliyepoulizwa kuhusu ukimya na hatua za maendeleo ya mchakato wa kufikia maridhiano ya Kitaifa na mahali zilipofikia .
Mbeto akijibu swali hilo,alisema kinachoendelea si ukimya juu ya ufumbuzi wa suala hilo, badala yake masuala yote kwa umuhimu wake ,yanaendelea kufanyiwa kazi huku yakifuata taratibu sahihi ,mazungumzo na uthabit wake.
Alisema Rais Dk Samia amekuwa akifuatilia na kuzingatia kila hatua , kwa ukaribu unaostahili pamoja na kuhakikisha makundi yote katika jamii, yanapata nafasi ya kushiriki ,kutoa maoni na kusikilizwa.
"Mchakato wa kufikia Maridhiano wenye lengo la kuponya yaliotokea ni kama zege .Zege likishachanganywa na kuwekwa kokoto, mchanga na saruji halilali.Rais bado yuko kazini usiku na mchana"Alisema Mbeto.
Aidha , Mwenezi huyo aliwaeleza Waandishi wa Habari waliofika Ofisini kwake kuulizia mchakato huo, alijibu akisema hatua zote zinazochukuliwa na Rais, zina baraka na kukiridhisha Chama Cha Mapinduzi .
"CCM na Serikali zake haziwezi kupuuzia jambo nyeti linalobeba maslahi na maisha ya jamii na kuliacha likibaki njia panda.Kazi inaendelea kwa kasi yenye kuridhisha na mchakato wake unaelekea kukamilika" Alieleza
Katibu huyo Mwenezi alisema hata hatua ya Rais kukutana na viongozi wa Vyama Vya Siasa, kamati ya Baraza la Maaskofu (TEC) ,Viongozi Wastaafu na Wanasheria ni katika juhudi za kufikia uponyaji unaokusudiwa.
Hata hivyo Mbeto alisifu mkakati wa Rais Dk Samia wa kuanzisha Tamasha la Kizimkazi ambalo ndani yake ,alisema limekuwa likijumuisha miradi dhidi umasikini ,kutumia fursa za elimu na uhamishaji wa miradi ya kijamii.
Alisema Tamasha hilo linajitanua kiutendaji kwa kufikia malengo yake na kuwepo ushiriki mkubwa wa jamii jambo huku likikuza haiba na taaswira ya kitaifa ,kikanda na kimataifa.
"Ubunifu na kuwepo Tamasha hili umeilenga jamii .Tamasha limejikita katika kupambana na maadui Ujinga,Umasikini na Maradhi. Limekuwa kioo na alama muhimu katika jamili "Alifafanua Mbeto.

0 Comments