Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, amemsifu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akisema uongozi wake umejikita katika utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja na kupanga miradi yenye maono ya muda mrefu kwa maendeleo ya Zanzibar.
Mbeto amesema hayo leo, Septemba 19, 2026, wakati akizungumza katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Mafunzo, Elimu na Michezo cha Tanzania Youth Icon (TAYI), Kikwajuni, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika hafla hiyo, Dkt. Mwinyi alikuwa mgeni rasmi.
Amesema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo unaoendelea nchini ni sehemu ya kutekeleza ahadi zilizotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Ilani yake, akisisitiza kuwa Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ina wajibu wa kuueleza na kuufafanua utekelezaji huo kwa wananchi.
Mbeto amesema Serikali chini ya Dkt. Mwinyi imeendelea kuchukua hatua katika maeneo mbalimbali, ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya michezo, elimu na huduma za kijamii.
«“Mheshimiwa Rais, kwa kweli Chama Cha Mapinduzi, shukrani zetu hazina mpango. Mheshimiwa Rais, umekuwa champion katika maeneo yote ambayo yameendelea. Tuliahidi kwenye Ilani kujenga viwanja kila wilaya, na tayari utekelezaji wake unaendelea,” amesema Mbeto.»
Aidha, Mbeto amesema uongozi wa Dkt. Mwinyi umeonesha mtazamo wa muda mrefu katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo, akisema Serikali imekuwa ikizingatia mahitaji ya wananchi ya sasa pamoja na ongezeko la mahitaji hayo katika miaka ijayo.
Amesema badala ya kuanzisha miradi kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo pekee, Serikali imekuwa ikipanga miradi yenye uwezo wa kuhudumia idadi kubwa zaidi ya wananchi hapo baadaye.
«“Kwa kweli Rais Mwinyi, mipango yake ni ya muda mrefu. Kama eneo linahitaji huduma ya watu elfu 10, sisi tunajenga mradi wa kuhudumia watu 50,000,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mbeto amempongeza Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, kwa juhudi zake katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.
Mbeto amesema Masauni amekuwa akifuatilia na kushughulikia masuala mbalimbali ya wananchi, ikiwemo changamoto zinazohusu huduma za maji na umeme.
Akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa umeme iliyowahi kuikabili baadhi ya maeneo ya jimbo hilo, Mbeto amesema Masauni alishiriki katika hatua za kutafuta suluhisho kwa wananchi.
«“Unakumbuka Mheshimiwa Rais, tulipata shida hapa, kukatika umeme mwezi mitatu mfululizo. Lakini Mheshimiwa Masauni yupo hapa, alihakikisha watu wa hapa wanapata maji. Mheshimiwa Masauni alichimba visima vikubwa na kusaidia wananchi,” amesema
Kituo cha Mafunzo, Elimu na Michezo cha TAYI kinatarajiwa kuwa sehemu ya kuwawezesha vijana kupata elimu, mafunzo, kukuza vipaji vya michezo pamoja na kujenga uwezo utakaowasaidia kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Hafla hiyo imefanyika ikiwa sehemu ya jitihada za kuweka mazingira bora kwa vijana kutumia vipaji, elimu, ujuzi na teknolojia katika kujenga maisha yao na kuchangia maendeleo ya Zanzibar.
Katika hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu, mafunzo, teknolojia, ajira na uwezeshaji wa vijana, akieleza kuwa mazingira rafiki kwa vijana ni muhimu katika kuhakikisha wanatumia uwezo wao kwa manufaa yao binafsi na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

0 Comments