MBETO AWATAKA MAWAZIRI SUK KUPIGANIA MASLAHI YA UMMA ZBAR



Na Mwandishi  Wetu, Zanzibar 

Chama Cha Mapinduzi kimesema kina matumaini na imani kubwa kwa Baraza la Mawaziri la Serikali  ya Mapinduzi  Zanzibar ilio chini ya  Umoja wa Kitaifa .

Vile vile , CCM kimewataka Mawaziri  toka  CCM na ACT ,kuthamini  uteuzi na  kulinda  heshima waliopewa na  Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi.

Tamko hilo limetamkwa na Katibu wa Kamati Maalum  ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi  ,Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis,  akiwa Afisini kwake Kisiwandui Kisiwani Unguja .

Mbeto alisema Mawaziri na Manaibu  wote wana jukumu  la  kulinda heshima waliopewa na Rais  ya kuitumikia Serikali na  wananchi kwa kusukuma mbele  gurudumu la maendeleo. 

Alisema  baada ya uteuzi wa Mawaziri na Manaibu   wake , kazi iliobaki  katika kila  Wizara,  ni  kumsaidia kazi  Rais ili afanikishe malengo ya kisera ya Serikali kwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi .

"Tunampongeza kwa dhati Rais Dk Mwinyi kwa uteuzi  na mabadiliko madogo katika  Baraza  lake .Kuna Mawaziri na Manaibu toka CCM na ACT .Tunachowahimiza wakawatumikie  Wananchi wote  " Alisema Mbeto .

Akielezea zaidi,  Katibu huyo Mwenezi  alisema kila Waziri dhamana ana wajibu wa kupigania maslahi ya Umma na  kuitumikia  Serikali  ya Umoja  wa Kitaifa kwa utii, uzalendo na  uaminifu mkubwa 

"Utaratibu mzima wa kuendesha Serikali unafahamika.Kila Waziri dhamana ana wajibu wa kutekeleza majukumu   ya kisera. Macho ya   wazanzibari  yanawatazama wao " Alieleza

Mbeto akisema kwa kusisitiza ,alisema huu ni wakati wa kuithibitisha dunia kuwa tashwishi za kisiasa, zinaweza kuwekwa kando ,na maisha yakaendelea bila mivutano 

"Twendeni tukajenge nchi. Maendeleo yanapotokea hayana alama za CCM au ACT.Itapendeza mawaziri wetu wakimudu kutenganisha Siasa na shime ya  Maendeleo " Alisisitiza Mwenezi huyo.

Akizungunzia kwa undani, Mbeto alisema maendeleo  ya nchi hayana alama ya siasa wala kiitikadi  ,badala yake maendeleo ya kisekta yakishamiri  hunufaisha watu wote .

Post a Comment

0 Comments