CUF YAADHIMISHA MIAKA 21YA WAHANGA WA MAUAJI YA JANUARI 2001

NA ABRAHAM NTAMBARA
MWENYEKI wa Chama Cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahimu Lipumba amewataka wanachama wa chama hicho kuwaenzi wahanga wa mauaji ya Januari 27 mwaka 2001 kwa kuendeleza mapambano ya kudai Demokrasia na haki nchini.
Kauli hiyo Profesa Lipumba ameitoa leo  wakati wa maadhimisho ya miaka 21 tangu kutokea kwa mauaji hayo, maadhimisho yaliyofanyika katika ofisi za Chama Buguruni jijini Dar es Salaam.
"Njia nzuri ya kuwakumbuka wenzetu waliofarili miaka 21 iliyopita ni kuhakikisha mapambano ya Demokrasia yanaendelea Bara na Zanzibar," amesema Profesa Lipumba.
Amesema haki sio ya kuombwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bali inapaswa kuendelea kupambaniwa na sio vinginevyo.
Aidha amesema kuwa chama kimepitia katika mengi hadi kupelekea baadhi ya wanachama wa chama hicho kuondoka, hivyo aliwaomba warejee ili waendelee kupambania haki kwani bado mapambano hayajakamilika.
Vile vile Profesa Lipumba amewataka wanachama kuhakikisha wanakiimarisha na kukijenga chama hicho kwa kukisambaza chama kwa wananchi kupitia ufunguzi wa matawi mapya yenye wanachama kuanzia 50 na kuendelea.
"Kuwaenzi ni kuhakikisha mapambano ya Demokrasia na haki yanaendelea ili kufanikiwa ni kuhakikisha tunapanua mtandao wa chama chetu," amesisitiza Profesa Lipumba.Katika hatua nyingine Profesa Lipumba amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuitisha mazungumzo ili kupata maridhiano ya kitaifa ambayo yataleta misingi imara ya Demokrasia ambayo itachochea maendeleo ya uchumi.





Post a Comment

0 Comments