Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza baada ya mapokezi Chanjo dhidi ya UVIKO-19 Aina ya Sinopham ambayo imefanyika katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
NA MWANDISHI WETU
SERIKALI ya Tanzania imepokea dozi 800,0000 ya Uviko-19 aina ya Sinopham
kwa ufadhili wa Serikali ya China.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam baada ya
mapokezi hayo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema dozi hizo zitatumika
kuchanya wananchi 400,000.
”Nichukue fursa hii kuishukuru Serikali ya China kwa kuwezesha
upatikanaji wa chanjo hizi. Hii ni awamu ya pili kwa chanjo za aina hii kutoka
Serikali ya China,” amesema Waziri Ummya.
Waziri Ummy ameleza kwamba awamu ya kwanza Tanzania ilipokea jumla ya
dozi 500,000 ambazo zilitumika kuchanja wananchi 250,000.
Amesema mapokezi ya chanjo hizo yanafanya jumla ya chanjo ambazo
zimeshapokelewa nchini tangu kuanza kutoa chanjo dhidi ya Uviko-19 hadi sasa
kuwa dozi milioni 8,821210 zikijumuisha Sinopham, Janssen, Moderna na Pfizer
ambazo zinatosha kuchanja jumla ya Watanzania milioni 5,082,380.
Akitoa taarifa ya hali ya Uviko-19 nchini, Waziri Ummy amesema hadi
kufikia Januari 23 mwaka huu jumla ya watu 33,000 wamethibitika kuwa na
maambukizi na watu 781 wamepoteza maisha.
“Natoa pole kwa wote waliopata madhara ya ugonjwa huu na waliopoteza
wapendwa wao. Serikali itaendelea kutoa chanjo dhidi ya Uviko-19 katika vituo
mbalimbali vya kutolea huduma ya Afya hapa nchini kwa mujibu wa miongozo
iliyopo,” amesema.
Amebainisha kuwa hadi kufikia Januari 25 mwaka huu jumla ya watu milioni
1,922,019 sawa na asilimia 3.33 ya Watanzania walikuwa wamepata chanjo kamili.
Amesema kati ya watu waliopata chanjo hizo hawajapata taarifa ya madhara
yoyote zaidi ya maudhi madogomadogo yaliyosababishwa na chanjo hzio .
“Hivyo basi chanjo hizi ni muhimu, salama na zimethibitika kuongeza
kinga ya mwili na kupunguza makali ya ugonjwa wa Uviko-19, kwa wale wanaopata
maambukizi,” ameongeza.
Amesema chanjo dhidi ya Uvico-19 imeshuhudiwa kuwa na ufanisi mkubwa
duniani kwa kupunguza makali ya ugonjwa ikiwemo kulazwa na kifo endapo mhusika
atakamilisha idadi ya dozi kwa wakati ulioshauriwa.
Ameeleza katika ufuatiliaji wa Serikali kuhusu taarifa za kuchajwa
miongoni mwa wagonjwa katika vituo vya huduma tangu Septemba mwaka jana,
imebainika kuwa idadi kubwa ya wanaolazwa na wanaokuwa na ugonjwa mkali au hata
kufariki ni wale ambao hawajapata chanjo.
Amesema kuanzia kipindi hicho hadi kufikia Januari 23 mwaka huu jumla ya
wagonjwa 3,147walilazwa ambapo 2,990 sawa na asilimia 95 walikuwa hawajachanja.
Aidha mesema kati ya wagonjwa mahututi 31 walioripotiwa Januari 23 mwaka
huu 30 sawa na asilimia 97 walikuwa hawajapata chanjo.
“Katika kipindi hiki jumla ya vifo 76 viliripotiwa ambapo vipo 73 sawa
na asilimia 97 vilikuwa vya wagonjwa ambao hawajachanjwa,” amesema.
Ameendelea kuwahimiza wananchi kupata chanjo ya Uvico-19 kwa kukamilisha
idadi ya dozi na kwa wakati kama inavyoshauriwa na wataalamu ili kujikinga.
mwisho
0 Comments