MRADI UJENZI MOROCCO SQUARE WAFIKIA ASILIMIA 93

NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imesema kuwa mradi wa ujenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wa Morocco Square umefikia asilimia 93.
Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete baada ya kufanya ziara ya kutembelea mradi huo kuona maendeleo yake.
“Mradi umefikia asilimia 93, unakaribia kwisha. Kilichokuwa kimeukwamisha ni upatikanaji wa fedha, hivyo kilichobaki nikutafuta hizo fedha ili kuukamilisha mradi na tumeshapewa ruhusa ya kuzitafuta,” alisema Kikwete.
Hata hivyo Kikwete alieleza kwamba ameridhishwa na maendeleo ya mradi huo na kuipongeza NHC kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kusimamia vizuri miradi yao inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.
Aliahidi kuhakikisha changamoto zinatatuliwa haraka ili mradi huo ukamilike.
“Mimi nimeridhishwa na mradi huu. Hivyo tuendelee kutafuta fedha ili mradi ukamilike. Na mimi kama Naibu Waziri nitahakikisha natoa ushirikiano utakaohitajika,” alisema Kikwete.
Aidha alisema ameitembelea NHC ili kutambua na kujifunza juu ya shirika hilo na kutambua changamoto linazokabiliana nazo na kuzitafutia ufumbuzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa NHC Maulidi Manyani alisema kwamba mradi unagharimu jumla ya shilingi bilioni 137.5 ambapo hadi sasa umeshagharimu shilingi bilioni 112.4.
Hivyo alisema kwa sehemu iliyobaki inahitaji shilingi bilioni 25.7 ili mradi ukamilike na kwamba upo mkakati wa kutafuta fedha hizo.

“Upo mkakati wa kuzitafuta fedha hizo, na tumeshapata ridhaa ya kuzitafuta,” alisema Banyani.

Post a Comment

0 Comments