Msanii Mrisho Mpoto (wa kwanza kulia) akisaini mkataba wa kuwa Balozi wa Kampuni ya JATU PLC kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya kutangaza miradi mbalimbali ya maendeleo.
NA ABRAHAM NTAMBARA
KATIKA kuunga mkono jitihada za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza na kuendeleza miradi ya maendeleo, Kampuni ya JATU (JATU PLC) imemteua rasmi kwa mara nyingine Balozi wao Mrisho Mpoto kuwa Balozi wa kampuni hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wakutiliana saini mkataba huo, Meneja Mkuu wa JATU PLC Mohamed Simbano amesema lengo ni kuendelea kutangaza miradi mbalimbali kama ya kilomo, ufugaji, maji, ujenzi na utalii inayofanywa chini ya uongozi wa Rais Samia.
"Tumeamua kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kumteua rasmi kwa mara nyingine Balozi wetu Mrisho Issa Hussen Mpoto kuwa Balozi wa JATU PLC kwa kipindi cha miaka mitatu kisha kumuandalia kipindi maalum kabisa cha KAA HAPA AWAMU YA PILI (KAA HAPA SEASON TU)," amesema Simbano.
Simbano ameeleza kuwa kipindi hicho kitakuwa kikifanyika kila siku ya Jumatano saa nne kamili usiku na marudio ni kila Jumanne saa tano kamili asubuhi kupitia Runinga ya Channel Ten.
Amesema Sekta ya Maji ni moja ya nguzo muhimu sana katika kuleta mapinduzi ya kilimo hususan kilimo cha umwagiliaji ambacho wamekuwa wakifanya katika mikoa mbalimbali ndani ya miaka mitano toka kuasisiwa kwa Kampuni ya JATU PLC.
"Kwa kweli tuna kila sababu ya kujivunia na kutembea kifua mbele tukiwa kama vijana tulio thubutu kwa kuishi ndoto zetu kwa kufanya kwa vitendo na kisha kuaminiwa na kilelewa na Serikali kwa kipindi chote cha miaka mitano," ameongeza.
"Maombi kwa Serikali yetu, ni muda sasa wakusapoti na kuishika mkono JATU PLC kwani hapa tulipofika haikua safari nyepesi hata kidogo na haitakuwa nyepesi kamwe, kwani ni dhahiri shahiri kuwa penye mafanikio hapakosi changamoto nasi changamoto kwetu ni fursa," amesema.
Ameongeza kwamba kwa miaka mitano wameweza kuingiza kampuni katika soko la hisa DSE, kufungua ofisi kikanda ndani ya nchi na Afrika Mashariki kwa kuanza na Kenya kwa ajili ya kupanua wigo wa masoko ya ndani na nje, kufungua kampuni ya Bima ya kilimo na ufugaji.
Vile vile ongezeko la wakulima zaidi ya elfu tano, kutoa ajira rasmi miatano na zisizo rasmi zaidi ya elfu kumi, kuchochea maendeleo ya Taifa kwa kulipa kodi mbalimbali na mwisho kukuza kipato kwa wanachama kwa kufanikiwa kuweka mifumo wezeshi.
Na kuweza kufanya kazi uwekezaji wa pamoja kupitia kampuni ya umma ya JATU PLC kwani asilimia 95 ya kampuni hiyo inamilikiwa na Watanzania tena wakawaida kabisa ambao wengi ni vijana, kina mama, makundi maalum, wazee pamoja na watumishi kutoka sekta tofauti tofauti.
Kwa upande wake Mpoto amesema amefurahi na kuishukuru Kampuni hiyo kwa kumpa mkataba huo mkubwa ambao utamuwezesha kutangaza miradi mbalimbali ya maaendelea na kuwawezesha wananchi kuijua.
"Nimefurahi sana, nashukuru kwa kupata mkataba huu mkubwa. Namshukuru Rais kwa kuniona na kunitengenezea njia na kuniwezesha kuonekana," amesema Mpoto. Februari 7 mwaka huu Serikali ilimteua Mpoto kuwa Balozi wa Wizara ya Maji.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya JATU PLC Mohamed Simbano (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kabla ya kuingia mkataba na Msanii Mrisho Mpoto (wa kwanza kulia) wa kuwa Balozi wa Kampuni hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu.
0 Comments