RAIS SAMIA AMUAPISHA DKT. MABULA, KUELEKEA UFARANSA NA UBELGIJI KWA ZIARA YA KIKAZI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Angeline Mabula kuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo amemuapisha Dkt. Angeline Sylvester Lubala Mabula kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Dkt. Mabula ameapishwa leo baada ya kuwa na udhuru wakati mawaziri wengine walipoapishwa mwezi uliopita.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Katika hatua nyingine, Rais Samia anatarajia kuondoka nchini kuelekea Ufaransa na baadae Ubelgiji kwa ajili ya ziara ya kikazi katika nchi hizo.

Akiwa nchini Ufaransa, Rais Samia anatarajiwa kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaojadili kuhusu Rasilimali Bahari Duniani.

Rais Samia pia atashuhudia utiaji Saini baina ya Serikali ya Tanzania na Ufaransa katika sekta za miradi ya maendeleo, ushirikiano katika masuala ya uchumi wa buluu, usalama wa bahari, sekta ya usafiri na maendeleo endelevu. 

Pamoja na masuala mengine, Rais Samia pia anatarajiwa kuzungumza na Watanzania waishio nchini Ufaransa.

 

 

Post a Comment

0 Comments