LHRC YAIPA TANO SERIKALI KUFUNGUA MLANGO WA MAJADILIANO KUHUSU SHERIA YA HABARI



Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Wakili Anna Henga.
NA ABRAHAM NTAMBARA
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeipongeza Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kufungua mlango wa majadiliano ya kuboresha Sheria ya Habari nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Wakili Anna Henga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kufuatia tamko la Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye lenye lengo la kufungua mlango huo kati ya Wizara ya Habari na wadau wa habari.

"Mheshimiwa Nape alitoa tamko hilo wakati wa Semina na Wahariri iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam katika makao makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)," amesema Wakili Henga.

Amebainisha kuwa Aprili 6 mwaka jana Rais Samia Suluhu Hassan wakati anaapisha safu ya makatibu na manaibu makatibu wakuu, na wakuu wa taasisi za Serikali alitoa agizo kwa iliyokuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kufungulia vyombo vya habari.

Kwamba Juni 28 mwaka jana pia wakati wa mkutano kati ya Rais Samia na Jukwaa la Wahariri Tanzania kuhusu siku 100 za uongozi wake alitoa agizo la kuweka mazingira mazuri kwa vyombo vya habari kwa kuwa hali haikuwa nzuri.

Amebainisha kwamba LHRC ikiwa mdau wa sheria za habari imefanya uchechemuzi kwa muda mrefu tangu kuibuka kwa wimbi la utungaji wa sheria zinazoweka ugumu kwa vyombo vya habari kufanya kazi zake.

"Pia kwa kiwango kikubwa Sheria hizo zimekwamisha urahisi wa upatikanaji wa taarifa kwa jamii. Miongoni mwa sheria hizo ni Sheria ya Makosa ya Mtandao, 2015, Sheria ya Upatikanaji wa Habari, 2016, Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano pamoja na kanuni zake, na Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari, 2016," amesema Wakili Henga.

Amesema kuwa Sheria hizo bado zipo na zimeendelea kuathiri utendaji wa vyombo vya habari, hivyo tamko la Waziri Nape ni kiashiria kizuri cha kurudi kwa uhuru wa vyombo vya habari na ni muda muafaka sasa kuangalia changamoto za kiujumla za sheria zinazoikabili Sekta ya habari na uhuru wa kujieleza.

"Tumeshuhudia kurejeshwa kwa leseni za magazeti manne ikiwemo gazeti la MwanaHalisi lenye leseni namba 0000433, Mawio lenye leseni namba 0000437, Mseto lenye leseni namba 0000436 na Tanzania Daima lenye leseni namba 0000434 kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan. Kiufupi, kumekuwa na maagizo ya Mahakama kuhusu kufunguliwa kwa magazeti yaliyofunguliwa," amesema.

Pamoja na hayo LHRC imetoa wito kwa Serikali kwamba kikosi kazi kitakachoundwa na Waziri kupitia upya na kutekeleza maamuzi ya Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya 2016.

Vile vile kuhakikisha mchakato wa maboresho ya sheria hizo unashirikiasha wadau wengi wa habari. Pia kufanya mapitio ya sheria zote zinazogusa sekta ya habari na upatikanaji wa taarifa nchini na kuweka mazingira rafiki ili kurejesha hali ya uchumi wa vyombo vya habari vilivyoathirika na sheria.

Kwa wadau wa habari Wakili Henga amewataka wadau wa habari kutoa maoni ya kina yatakayochangia kuboreshwa kwa sheria za habari.

Post a Comment

0 Comments