MGANGA MKUU DAR AWASHUKURU VIONGOZI WA DINI KWA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO-19

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume

NA ABRAHAM NTAMBARA

MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume amewashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika mapambano ya Uviko-19 kwa kuhamasisha wananchi kuchanja.

Shukurani hizo alizitoa akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Qaswida za ujumbe wa Uviko-19 (Corona 2022).

“Kubwa ni kuendele kuwashukuru viongozi wa dini na nitoe rai kwa viongozi wengine pia wa dini mbalimbali wa madhehebu mbalimbali kuiga hiki kitendo kizuri ambacho kinafanyika,” alisema Dkt. Mfaume.

“Matokeo ya kuwaunganisha viongozi wa dini katika hizi hamasa za kupambana na Uviko-19 tumeona mfano hata kwenye uchanjaji Mkoa wa Dar es Salaam idadi ya watu ambao wananchanja kwa siku imeongezeka sana. Kwa sasa tunachanja hadi watu 6000 kwa siku,” aliongeza.

Akizungumzia kuhusu mashindano hayo ya Qaswida alisema kuwa Januari 21 mwaka huu walikutana na viongozi wa dini na kuwaomba waangalie ni namna gani watatoa mchango wao katika kuhakikisha wanawahamasisha wananchi kuchanja.

Hivyo aliwashukuru Bakwata kupitia Jumuiya yake ya Vijana kwa kuja na ubunifu huo kwani licha tu ya vijana hao kushiriki mashindano hayo bali yataweza kutoa elimu kwa wananchi na hatimaye kuwasukuma kupata chanjo ya Uviko-19.

“Leo hii tukio ambalo liko mbele yetu tuna uzinduzi wa uimbaji wa Qaswida wenye jumbe mbalimbali za kupambana na Uviko-19, na sisi hapa kama Serikali kwa kweli tuendelee kuwashukuru sana viongozi wetu wa Dini.

“Tulikutana nao Januari 21 mwaka huu, tukawaomba watusaidie kwa namna wanavyojua kuanzisha aina ya ubunifu ambao wanaujua wanaoweza wakaufanya ili watusaidie kufikisha jumbe mbalimbali kwa waumini lakini kupitia kwa waumini naamini kwamba jamii nzima itakuwa imepata ujumbe,” alisema.

Aidha Dkt. Mfaume aliwashukuru wadau wa maedeleo wakiwemo Shirika la MDH kwa kuunga mkono jitihada hizo.     

 “Na kwa keli nichukue nafasi hii kuwashukuru wenzetu wa MDH hawakusita kuwasapoti wenzetu viongozi wa dini baada ya kuona kwamba mara nyingi viongozi wa dini wanapopata fursa wanapowezeshwa wamekuwa ni wa msaada mkubwa,” alisema.

Aidha kwa vijana waliojitokeza kushiriki mashindano hiyo Dkt. Mfaume aliwataka waendelee kutiwa moyo kwa sababu kwa wao ni mashindano lakini kama Serikali inaangalia thamani ya wao kushiriki na ujumbe ambao watautoa kwenye mapambano dhidi ya Uviko-19.

“Kwa hiyo tumewasihi kati ya wale ambao bahati mbaya hawataweza kupata fursa ya kushinda katika hatua nyingine wasikate tamaa, tunawategemea sana wakatufikishie jumbe hizo, wananchi waendelee kuchukua tahadhari ya matumizi ya barakoa, matumizi ya Sinitizer na kuchanja,” alisema.

Kwa upande wake Msimamizi wa Miradi yote ya MDH kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam Ally Kaduma alimshukuru Mgang Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Bakwata kupitia Sheikh Pembe kwa kuwaunganisha katika kupambana na Uviko-19.

”Mnajua kwamba sasa hivi tuna kwenda kwenye jamii na mkumbuke na Jamii inalinwa na Dini inalinwa na Imani na Imani inasimamiwa na Dini. Na Dini moja wapo ambayo inasimamia Imani yetu Dini ya Kiislam na Bakwata ni Baraza ambalo linasimamia Imani yetu,”.

Hivyo alisema kama MDH wanashirika kwa sababu wanakwenda kupambana na virusi vya Corona, kwamba Bakwata wamejitolea kuwa mstari wa mbele katika mapambano hivyo na wao wapo kwa ajili ya kuwaunga mkono.

 


Post a Comment

0 Comments