Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ACP Muliro Jumanne Muliro
NA MWANDISHI WETU
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia mtu mmoja kwa kujifanya Askari Polisi.
Hayo yalibainishwa jana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaa ACP Muliro Jumanne Muliro alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Kamanda Muliro alisema kuwa tukio hilo limetokea Februari 9 mwaka huu majira ya saa sita na nusu mchana huko maeneo ya Vingunvguti Mtakuja ambapo alikamatwa Hussein
Alimtaja mtu huyo kuwa Ramadhani, miaka 30, Mzaramo na mkazi wa Sinza ambaye akiwa amevaa sare za Jeshi la Polisi (Jungle Green) akijifanya Askari Polisi alikuwa akikamata watu ovyo huku wakati mwingine akijihusisha na matendo ya unyang`anyi wa kutumia nguvu akiwa amevaa sare hizo.
“Upekuzi zaidi ulimkuta akiwa na vifaa vimgine kama Buti za Jeshi la Polisi, kadi za Benki NMB na CRDB, kadi ya Mpiga kura na kadi za NSSF zenye jina la Florence Victor Kiondo ambazo zinachunguzwa jinsi alivyozipata na kuhusishwa na tukio la kihalifu.
Hata hivyo Kamanda Muliro alisema kuwa kumbu kumbu zinaonesha mtuhumiwa huyo alishawahi kufungwa kwa makosa mbalimbali na taratibu za kisheria zinafanyika ili kumfikisha tena Mahakamani.
“Mtuhumiwa alishawahi kufungwa jela miaka 4 CC no 138/2018 kwa kosa la kujeruhi akatumikia kifungo katika Magereza ya Mkuza Kibaha, Rwanda Mbeya na kumalizia kifungo Gereza la Kitai Mbinga Mkoani Ruvuma. Pia alishawahi kuhukumiwa kifungo nje miezi 6 na Mahakama ya Mwanzo Buguruni CC NO 893/2021 tarehe 19/08/2021 kwa kosa la wizi,” alisema.
Alisema Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam litaendelea kufuatilia watu mbalimbali wanaojifanya watumishi wa mamlaka za Serikali na kuwabughudhi raia wakati wao si mamlaka hizo husika
Katika hatua nyingine , Kamanda Muliro alisema kuwa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam eneo la Kariakoo Mtaa wa Msimbazi na Livingstone limemkamata Maila Majula, Mjita, Mkristo, miaka 29, Biashara, mkazi wa Makongo juu kwa kutoa taarifa za uongo katika kituo cha Polisi Msimbazi za kuibiwa Gari lake namba T.303 DPS aina ya Toyota IST rangi ya Bluu.
“Uchunguzi umebaini kuwa mtuhumiwa alipewa T.shs Milioni kumi na kaka yake ili akaziweke Benki matokeo yake akazitunia kwa matumizi yake binafsi na kuamua kutengeneza tukio la kufkikirika kuwa pesa ile na gari viliibwa wakati yeye aliposhuka kwa muda na aliporudi hakukuta gari iliyokuwa na pesa,” alisema.
Kwamba baada ya kumtilia mashaka mtoa taarifa ilibainika kuwa taarifa hizo ni za uongo, na ilibainika gari hilo alikuwa amelificha maeneo ya Tabata kwa Swai ambako lilipatikana kabla ya kwenda kituoni kutoa taarfa za kuibiwa kwa Gari hilo.
0 Comments