Mwenyekiti wa Binti Shupavu Hadija Seif akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Msasani A iliyopo wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam.
Bondia wa Kimataifa wa Tanzania Selemani Kidunda akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Msasani A iliyopo wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Kata ya Msasani wilayani Kinondoni Mkoani Dar es Salaam akizungumza na wanafunzi wa shule ya Msingi Msasani A wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam (aliyevaa nguo ya njano).
Habari katika picha
NA ABRAHAM NTAMBARA
TAASISI ya Binti Shupavu imetoa elimu
ya hedhi salama kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Msasani ‘A’ iliyopo wilayani
Kinondoni mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu
hiyo ulioambatana na utoaji wa msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi hao,
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Hadija Seif ambaye pia ni mwandishi wa habari wa
Michuzi Media amesema kuwa lengo lao ni kuona mabinti wanakuwa shupavu na
kupinga vishawishi ambavyo vitawafanya kutotimiza ndoto zao.
“Kwanini Binti Shupavu, lengo ni kuona
mabinti wanakuwa shupavu na kusimama wenyewe na kupinga vishawishi, tunaangalia
wasichana ambao wanapata vishawishi na kukatiza ndoto zao,” amesema Hadija na
kuongeza kwamba,
“Tupo tayari kukemea hivyo vishawishi
na kuwaambia mviepuke ili mfikie ndoto zenu,”.
Amewataka wanafunzi hao kuwa huru
kumweleza mzazi/mlezi wa kiume wanapokuwa katika kipindi cha hedhi ili waweze
kupata huduma stahiki ikiwemo kununuliwa taulo za kike.
“Na unatakiw akujenga urafiki na ndugu
zako wa damu, kama vile baba, mama, mjomba, bibi, shangazi na sio watu wengine
wakiwemo bodaboda ambao watakuingiza katika vishawishi hatarishi,” amesema
Hadija.
Kwa upande wake Mwanamasumbwi wa
Tanzania Selemani Kidunda akizungumza kwa niaba ya akina baba, amesema kwamba
Binti Shupavu ni yule ambaye anajiamini na mwenye uwezo wa kuepuka vishawishi
hatarishi.
Aidha amewataka watoto
wa kike kutambua kwamba hedhi sio ugonjwa na kwamba wanapokuwa katika kipindi
cha hedhi wasiogope kuwaambiwa wazazi wao yaani baba na mama.
“Baba ni kama mama
usiogope kumwambia, ukipata tatizo mshirikishe ili akusaidie,” amesema Kidunda.
Naye Afisa Ustawi wa
Jamii Kata ya Msasani wilayani Kinondoni Mkoani Dar es Salaam, Kichiki Njovu
amewataka watoto wakike wanapokuwa na tatitizo wasiwaeleze watu wa barabarani
na badala yake wawaambie wazazi au waalimu kwa msaada zaidi.
“Usimwombe msaada mtu yeyote
barabarani mfano bodadoda kwani hata kupa msaada bure. Mwisho wake utapata
ujauzito na kushindwa kutimiza ndoto zako kwani hedhi ni chanzo cha kupata
ujauzito,” amesema na kuongeza kuwa,
“Kwahiyo sasa hivi
ukikutana na mwanaume utapata ujauzito, ukipata ujauzito nani atakutunza,
unakuta wazazi wengine ni wakali wanakufukuza,”.
Hivyo amewataka watoto
hao wakike wajitunze kwamba wasikimbilie kupata mimba za utotoni.
0 Comments