Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa kutoka Tume
ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Samson Mwela (picha ya kwanza juu) akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
NA ABRAHAM NTAMBARA
TUME
ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imepokea ugeni wa watu 35
kutoka Chuo Kikuu cha Northeastern kilichopo Boston nchini Marekani ambao
umekuja kwa ajili ya kujadiliana kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto za
mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 1, 2022 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa kutoka COSTECH Samson Mwela amesema ugeni huo pia utatumia fursa ya ujio wao kujifunza hali ya mabadiliko ya tabianchi nchini.
Mwela ameongeza kwamba kupitia mkutano na wageni hao watajadiliana namna ya kushirikiana kwa pamoja kupitia program wanazojifunza chuoni ili kuweza kutatua changamoto hiyi ya mabadiliko ya tabianchi.
Aidha amesema kuwa kupitia majadiliano hayo wataimarisha mahusiano kati ya Chuo hicho cha nchini Marekani pamoja na vyuo vya hapa nchini jambo litakalosaidia kuimarisha ufanyaji wa tafiti za kisayansi zenye lengo la kusaidia kutokomeza madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.
“Marekani wanateknolojia na maarifa hata sisi pia tunayo hivyo leo tunajifunza kutoka kwao na wao wanajifunza kutoka kwetu na tumewaalika Chuo cha Maji, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu na kuja na makubaliano ya pamoja ya namna ya kutatua changamoto hizi za mabadiliko ya tabianchi” Amesema Mwela.
Ameongeza kuwa Sayansi na Teknolojia inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi wa Taifa hivyo COSTECH kama waratibu wakuu wa Sayansi, teknolojia na ubunifu wanao wajibu wa kuwaunganisha watafiti wa ndani na nje ya nchi ili wafanye tafiti zenye tija kwa maslahi ya Taifa.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) Dkt. Khadija Malima amesema kutokana na program ya pamoja ya wanafunzi inayofanywa na Chuo hicho cha nchini Marekani ujio wao utasasidia kuleta hamasa kwa vyuo vya hapa nchini.
Amesema kwamba majadiliano hayo pia yatasaidia kutambua namna mabadiliko ya Tabianchi yanavyoathiri afya ya Binadamu hususani katika janga linaloisumbua dunia kwa sasa la Uviko-19.
Naye Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Ladislaus Chang’a amesema ushirikiano huo utaenda kujibu namna tunavyoweza kushirikiana katika tafiti na kukabiliana na matatizo ya tabianchi.
0 Comments